Owen: Shearer? Sina stori naye
Muktasari:
- Shearer alitaka kumwanzisha straika Owen kuwa na nafasi nzuri ya kupata matokeo mazuri, lakini staa huyo wa zamani wa England amesema hakuwa kwenye kiwango bora kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa anatoka kuwa majeruhi.
NEWCASTLE, ENGLAND: MICHAEL Owen amesema amekuwa hazungumzi na Alan Shearer baada ya kudai alifanya makosa kumkosoa wakati alipokuwa akicheza chini yake huko Newcastle United.
Owen alicheza chini ya Shearer huko Newcastle katika msimu wa 2008-09 na timu hiyo ilishuka daraja.
Newcastle ilishuka daraja baada ya kuchapwa 1-0 na Aston Villa, wakati ilihitaji pointi moja tu isishuke.
Shearer alitaka kumwanzisha straika Owen kuwa na nafasi nzuri ya kupata matokeo mazuri, lakini staa huyo wa zamani wa England amesema hakuwa kwenye kiwango bora kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa anatoka kuwa majeruhi.
Owen aliingia dakika 25 za mwisho katika mchezo huo kabla ya Newcastle kushushwa hadi kwenye Championship.
Miaka kadhaa baadaye, Shearer alidai Owen angefanya zaidi kusaidia timu kubaki kwenye ligi. Kisha aliongeza kusingekua na maana yoyote kama Owen angepata majeraha kwa sababu msimu ndiyo kwanza ulikuwa unakwisha.
Owen amekuwa akificha kuwapo na malumbano baina yao na walicheza pamoja kwenye kikosi cha England na Newcastle katika msimu wa 2005-06 na siku zote wamekuwa wakiheshimiana.
Lakini, amesema wamekuwa hawazungumzi na bado hakubaliani na maneno yake. Amesema: “Ninapokutana na Shearer tunashikana mikono tu, hatuna maongezi, tumeamua kuwa hivyo. Namheshimu, lakini alikosea kusema alichosema.”