Ombi la Crystal Palace lagonga mwamba EPL
Muktasari:
- Palace ilitaka mechi hiyo ipangwe Jumamosi ili kupata muda zaidi wa kujiandaa na fainali ya Conference League dhidi ya Rayo Vallecano, Jumatano ijayo.
Ligi Kuu ya England (EPL) imekataa ombi la Crystal Palace kutaka mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Arsenal ichezwe Jumamosi hii badala ya Jumapili.
Palace ilitaka mechi hiyo ipangwe Jumamosi ili kupata muda zaidi wa kujiandaa na fainali ya Conference League dhidi ya Rayo Vallecano, Jumatano ijayo.
Hata hivyo, uongozi wa ligi umesisitiza kuwa mechi zote 10 za kufungia msimu lazima zichezwe wakati mmoja, Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni, ili kulinda usawa na uadilifu wa mashindano hayo.
Kocha wa Crystal Palace, Oliver Glasner, amekiri kuwa walijaribu bahati yao kwa kuwa Arsenal tayari imeshanyakua ubingwa wa ligi, hivyo mechi hiyo haina madhara kwenye msimamo wa ligi.
"Tulijaribu kusogeza mbele mchezo huu kwa sababu ungetusaidia kupata siku moja zaidi ya mapumziko kuelekea Jumatano. Kwa sababu wapinzani wetu Vallecano wanacheza Jumamosi jioni, kwa hiyo watapata muda mzuri wa kupumzika," amesema Glasner.
Ameongeza kuwa hakuwa na kinyongo na uamuzi huo akielewa kuwa kuna masuala ya mikataba ya haki za matangazo ya TV na maandalizi ya Arsenal kukabidhiwa kombe lao katika uwanja wa Selhurst Park.
Mchezo huo wa keshokutwa Jumapili utakuwa wa mwisho kwa Glasner kama kocha wa Crystal Palace, akiondoka kama kocha aliyepata mafanikio makubwa zaidi klabuni hapo.
"Sitaondoka kwa hasira, umekuwa mchakato wa wiki na miezi kadhaa. Nilihisi ni wakati sahihi wa kutafuta changamoto mpya. Nitawakumbuka sana watu na mashabiki wa hapa," amesema kocha huyo mwenye umri wa miaka 51.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Glasner amempongeza mchezaji wake wa zamani, Eberechi Eze, ambaye atarejea Selhurst Park keshokutwa Jumapili akiwa na kikosi cha Arsenal na atapata fursa ya kunyanyua taji la Ligi Kuu.
Eze, aliyebakisha historia Palace kwa kufunga bao la ushindi la FA Cup msimu uliopita, alikaribia kujiunga na Tottenham msimu uliopita wa kiangazi kabla ya kusajiliwa na Arsenal kwa kitita cha pauni milioni 60.
Glasner alitania kuwa Eze alifanya uamuzi sahihi kwenda Arsenal kuliko klabu nyingine (akilenga Spurs ambayo inakabiliwa na hatari ya kushuka daraja), huku Arsenal ikitwaa ubingwa wao wa kwanza baada ya miaka 22.
Kocha huyo amemalizia kwa kusifu juhudi za wachezaji wake nyota wa zamani, akiwemo Eze, Marc Guehi (aliyeenda Man City), na Michael Olise (aliyeenda Bayern Munich).
"Wana vipaji vikubwa, lakini tabia yao ya kufanya kazi kwa bidii ndiyo inayowafanya wawe mastaa wakubwa. Eze alikuwa akibaki uwanjani baada ya mazoezi kufanya mazoezi ya kufunga, na Marc alifanya vivyo hivyo kwenye kuzuia na kupiga pasi. Ninajivunia kufanya kazi nao."