Olmo, Pau wamkasirikia rais Barca
Muktasari:
- Mastaa hawa wawili wanakutana na hali ya sintofahamu kwani kwa sasa hawajaingizwa tena katika mfumo na hawawezi kuchezea Barcelona katika kipindi kilichobakia cha msimu huu, linaripoti gazeti la AS.
BARCELONA, HISPANIA: NYOTA wa Barcelona Dani Olmo na Pau Victor wanaripotiwa kuwa na hasira na rais wa timu hiyo Joan Laporta baada ya Barca kushindwa kuwaandikisha tena wachezaji hao.
Mastaa hawa wawili wanakutana na hali ya sintofahamu kwani kwa sasa hawajaingizwa tena katika mfumo na hawawezi kuchezea Barcelona katika kipindi kilichobakia cha msimu huu, linaripoti gazeti la AS.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Olmo na Victor wamekasirishwa sana na Laporta baada ya juhudi za Barcelona za kuwaandikisha tena katika ligi kukataliwa na La Liga na Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF), wakiamini kiongozi huyo ameshindwa kufanya kazi yake kwa ufasaha hali iliyosababisha jambo hilo kutopatiwa ufumbuzi hadi sasa.
Mbali ya Olmo na Viktor, inaelezwa mashabiki wa Barcelona pia wameonyesha hasira zao dhidi ya Laporta na kumtaka ajiuzulu kutokana na suala hili.
Wachezaji kwa sasa hawatotumika na Barcelona ambayo imetoa taarifa kuwa imewasilisha kesi mahakamani na walikosekana pia katika mchezo wa Kombe la Copa del Rey dhidi ya Barbastro.
Hata hivyo, licha ya mpango wa Barcelona kupeleka kesi hiyo mahakamani kupinga uamuzi wa La Liga na RFEF, taarifa zinaeleza suala hilo lina asilimia chache sana za kufanikiwa,
Barca imefikia hatua hiyo kutokana na hali ya kiuchumi ambayo inawataka kwanza kuwasilisha vielelezo vinavyoonyesha uchumi wao umeimarika ili kuweza kuwaingiza wachezaji hao tena katika mfumo.
Sheria za kifedha za La Liga zinazitaka timu kutumia sawa na inachokiingiza na Barca imefikia ukomo wa matumizi yake na ili kuweza kuingiza mchezaji katika mfumo itahitaji aidha kuuza wachezaji waliopo ama kutafuta pesa za udhamini ili kuweza kuwaandikisha.