Nunez, Barcelona imefikia patamu

Muktasari:

  • Kitendo hicho kimezidisha tetesi za kuondoka kwake dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

IKIWA ni siku chache tangu ahusishwe na Barcelona, mshambuliaji wa Liverpool, Darwin Nunez, 24, amefuta picha zote alizopiga akiwa Anfield katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Kitendo hicho kimezidisha tetesi za kuondoka kwake dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Barcelona inataka kumsajili Nunez dirisha lijalo ili akachukue nafasi ya Roberto Lewandowski ambaye wamepanga kumuuza ili kupunguza gharama za uendeshaji wa timu.

Viongozi wa Barca wanaamini gharama hizo zitapungua kwa sababu Lewandowski ni kati ya wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa.

Tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi timu kibao kutoka Saudi Arabia zimekuwa zikiulizia uwezekano wa kumsajili staa huyu lakini zilifeli.

Nunez anaweza kuwa tayari kuondoka kwa sababu Jurgen Klopp ambaye ndio alipambana asajiliwe naye anaondoka.

Mkataba wa Nunez   unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, msimu huu amefunga mabao 18 na kutoa asisti 13, katika mechi 52 za michuano yote.

Inter Milan imepanga kusikiliza ofa kutoka timu mbalimbali ili kumuuza beki wao raia wa Uholanzi, Denzel Dumfries, katika dirisha lijalo la maira ya kiangazi. Timu kibao zinahitaji saini ya staa huyu ikiwemo Manchester United. Dumfries mwenye umri wa miaka 28, ni mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Inter na msimu huu amecheza mechi 34 za michuano yote na kutoa asisti sita.

CHELSEA imegonga hodi kwa Shakhtar Donetsk wakihitaji saini ya kiungo wa timu hiyo na Ukraine, Georgiy Sudakov, 21, ambaye taarifa kutoka Daily Mail zinaeleza anaweza kuuzwa kwa zaidi ya Pauni 65 milioni. Mbali ya Chelsea, Sudakov pia anawindwa na  Arsenal, Manchester City na Liverpool.  Chelsea huenda ikamtumia staa wao raia wa Ukraine, Mykhailo Mudryk kwa ajili ya kumshawishi Sudakov atue katika kikosi chao.

CHELSEA ipo tayari kulipa Pauni 100 milioni kwa ajili ya kumsajili straika wa Napoli, Victor Osimhen katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kwa mujibu wa tovuti ya Skysports, katika mkataba wa Osimhen kuna kipengele ambacho kinamruhusu kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa timu inayomhitaji italipa zaidi ya Pauni 100 milioni na huenda dili hilo likakamilishwa.

ROMA imepanga kumnunua mazima straika wa Chelsea, Romelu Lukaku katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kuvutiwa na kiwango alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Lukaku ambaye anacheza Roma kwa mkopo pia anawindwa na baadhi ya timu za Saudi Arabia zilizoanza harakati za kutaka kumsajili tangu dirisha lililopita la majira ya baridi.

KIPA wa Atletico Madrid na Slovenia, Jan Oblak, 31, yupo kwenye rada za Chelsea inayotaka kumsajili kwa ajili ya kuongeza ushindani zaidi katika eneo lao la kipa. Chelsea imeshawishika kumsajili Oblak baada ya Atletico wenyewe kudaiwa kuwa katika mpango wa kuuza baadhi ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza kwa ajili kupata pesa za kufanyia maboresho timu yao.

NEWCASTLE imepanga kuingia vitani dhidi ya Manchester United na Manchester City kumsajili winga wa Crystal Palace, Michael Olise na timu yake inataka zaidi ya Pauni 60 milioni ili kumuuza mwisho wa msimu. Olise amezidi kuchanganya vigogo Ulaya kutokana na kiwango alichoonyesha msimu huu hususani mechi hizi za mwishoni.

WEST Ham na Tottenham zimepanga kuwasilisha ofa ya Pauni 50 milioni kila mmoja ili kuipata saini ya straika wa Brentford, Ivan Toney, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Toney ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwakani, amekuwa akihusishwa pia na Chelsea na Arsenal.