Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Novatus Dismas kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya

MIAKA mitatu iliyopita ilikuwa katika hafla ya ugawaji Tuzo za Ligi Kuu Bara pale Mliman City baada ya msimu wa 2019/20 kumalizika ambao Simba ilitwaa ubingwa ikiwa ni mara ya tatu mfululizo, nilipata nafasi ya kufanya mahojiano na Novatus Dismas Miroshi.

Ilikuwa ni baada ya mchezaji huyo aliyekuwa akiichezea kwa mkopo Biashara United ya Mara kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu huku akiwapiga bao, Kelvin Kijiri aliyekuwa KMC na Dickson Job wakati huo alikuwa Mtibwa Sugar.

Novatus alionyesha wazi shauku ya kucheza soka la kulipwa Ulaya kama ilivyokuwa kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye wakati huo ndio alikuwa ametua zake England na kusajiliwa na Aston Villa baada ya kufanya makubwa KRC Genk.

“Bro (Eliya) ni ndoto yangu kucheza Ulaya, naamini ipo siku milango ya kheri itanifungukia na kupata hiyo nafasi,” alisema miaka mitatu iliyopita, akiwa amevalia suti yenye rangi ya damu ya mzee.

Tangu hapo tulibadilishana namba na mchezaji huyo na nilikuwa nikimpa moyo huku nikimpa ushuhuda wa wachezaji wengi wa Kitanzania walivyofanikiwa, yote hiyo ni kutokana na ufuatiliaji wangu wa wachezaji ambao wanacheza nje ya nchi ambao nimekuwa nikiwaripoti kwenye safu hii ya Nje ya Bongo.

Mara baada ya kuwa na msimu mzuri na Biashara United ambayo aliisaidia kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tisa huku ikiwa imejikusanyia pointi 50, waajiri wake, Azam FC walimrejesha kwenye mipango yao kwa ajili ya msimu uliofuata wa 2020/21.

Nakumbuka nilionana naye tena kwenye tamasha la Azam FC ambapo alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotambulishwa lakini ni bahati iliyoje kwake kwani milango ya safari ya kuifuata michuano mikubwa zaidi Ulaya ngazi ya klabu ilifunguka.

Ilikuwaje? Alipata mwaliko wa kwenda kujifunza Israel kwenye Klabu ya Maccabi Tel Aviv lakini baadaye akapata nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi cha vijana cha timu hiyo na ndipo walipovutiwa naye kisha wakakaa chini na Azam FC ambao kwa roho nyeupe walibariki safari ya kijana wao kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Ndani ya mwaka mmoja tu, Novatus alipandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya soka la Israel lakini kutokana na changamoto ya namba hakucheza mchezo hata mmoja ikabidi apelekwe kwa mkopo Beitar Tel Aviv Bat Yam ambayo ilivutiwa naye.

Novatus alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na timu ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 20 Februari 16, 2021 katika kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Ghana kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya fainali za Mataifa ya Afrika la U-20 2021.

Septemba 2,  2021, nyota huyo alicheza mechi yake ya kwanza katika sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo katika kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA la 2022 huku Septemba 7, akifunga bao lake la kwanza katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Madagascar na hapo ndipo nilipofanya naye mahojiano mengine ya ana kwa ana.

Alionekana kuwa Novatus tofauti na yule ambaye tulikutana mara  ya kwanzaa pale Mlimani City, uso wake ulijieleza, Ulaya ilikuwa imeanza kumkubali ni kama alianza kung’aa hivi kimtindo, nilimpongeza kwa hatua ambazo anaendelea kupiga.

“Nilikuwambia bro (Eliya), napambana kuhakikisha nacheza mpira kwenye ligi kubwa zaidi Ulaya,” alisema.

Hatukuishia hapo, alinialika Kinyerezi ambako alikuwa akikaa na washikaji zake akiwemo Mohammed Rashid ambaye aliwahi kufanya vizuri Ligi Kuu akiwa na Tanzania Prisons na Simba, alipenda kukaa huko kwa ajili ya utulivu zaidi huku akisubiri kurejea zake Ulaya.

Mwaka mmoja ulitosha kucheza soka Israel alipata shavu la kwenda Ubelgiji ambako alijiunga na Zulte Waregem, aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku akianza kutumika kama beki wa kati kwenye ukuta wa mabeki watatu nyuma na baadaye akawa anacheza kama beki wa kushoto fofauti na namna ambavyo tulizoea kumwona akicheza kama kiungo mkabaji au mchezeshaji.

Uwezo wake wa kukaa mpira mguu ulimfanya kunoga zaidi kwenye nafasi hizo kwani makocha wengi wanapenda kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma hivyo alinoga katika maeneo tofauti ambayo alitumika.

Licha ya Zulte Waregem kushuka daraja lakini Novatus alionyesha kiwango kikubwa kiasi cha kuhusishwa na timu mbalimbali ikiwemo za Ligi Daraja la Kwanza England ‘Championship’.

Wakati ambao akili na mawazo yake ikiwa ni kuipambania Zulte Waregem kuhakikisha inarejea Ligi Kuu Ubelgiji huku akitumika kwenye michezo ya mwanzoni ndipo ilipoibuka ofa siku ya mwisho kabla ya dirisha la usajili kufungwa alitua zake Ukraine kwa ajili ya kujiunga kwa mkopo wa msimu mzima na Shakhtar Donetsk wenye kipengele cha kusajili jumla.

Akili yake iliwaza fursa iliyopo mbele yake ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwa bahati nzuri alipata baraka zote kutoka kwa wajiri wake.

“Nilihisi ni kama nipo ndotoni vile, huu ndio ukuu wa Mungu kile ambacho nilikuwa nikikiota hatimaye kimetimia,” anasema Novatus ambaye wiki iliyopita alikuwa Mtanzania wa pili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya nyuma ya Samatta aliyefanya hivyo akiwa na KRC Genk.

Novatus amefanya hivyo akiwa na umri wa miaka 21 bado ana nafasi ya kufanya makubwa zaidi na huenda baada ya miaka michache ijayo tukamshuhudia akicheza katika moja ya nchi kubwa zaidi kwenye soka la Ulaya kama vile Ujerumani, Italia, Ufaransa na hata ikiwezekana England. Kweli kila kitu ni dhamira na kujituma. Kila la kheri Novatus.