Spence akwepa kusalimiana kwa mikono na Partey
Muktasari:
- Ingawa si salamu zote zilionyeshwa kwenye matangazo ya moja kwa moja ya televisheni, lakini video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mchezaji huyo wa Tottenham Hotspur akionekana kumpita Partey bila kumpa mkono wakati wa utambulisho wa wachezaji kabla ya mchezo huo wa Kundi L.
Beki wa England, Djed Spence, ameonekana kutomsalimia kwa mkono kiungo wa Ghana, Thomas Partey, kabla ya mechi ya Kombe la Dunia iliyochezwa kati ya timu hizo.
Ingawa si salamu zote zilionyeshwa kwenye matangazo ya moja kwa moja ya televisheni, lakini video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mchezaji huyo wa Tottenham Hotspur akionekana kumpita Partey bila kumpa mkono wakati wa utambulisho wa wachezaji kabla ya mchezo huo wa Kundi L.
Wachezaji wa England walionekana kumsalimia Partey kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa kabla ya mechi, lakini Spence alimkwepa huku akiwasalimia nyota wengine wa Ghana.
Kabla ya mchezo huo, Chama cha Soka England (FA) hakikutoa mwongozo maalumu kwa wachezaji wake kuhusu namna ya kushughulikia kukutana na Partey wakati wa hafla ya kabla ya mechi hiyo mjini Boston, Marekani.
Hata hivyo, matarajio yalikuwa kwamba wachezaji wote wa England wangefuata taratibu za FIFA za kusalimiana na wapinzani wao, kama walivyofanya walipocheza dhidi ya Croatia jijini Dallas, wiki iliyopita.
Haya yanajiri wakati huu ambao Partey mwenye umri wa miaka 33, anakabiliwa na mashtaka saba ya ubakaji na shtaka moja la unyanyasaji wa kingono, yanayohusiana na madai yaliyotolewa na wanawake wanne tofauti kati ya mwaka 2020 na 2022. Mchezaji huyo amekanusha mashtaka yote na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mwaka 2027.
Kiungo huyo wa Villarreal ya nchini Hispania, hakushiriki mchezo wa kwanza wa Ghana kwenye Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Canada baada ya maafisa wa Canada kumzuia kuingia nchini humo.
Baada ya kuikosa mechi hiyo, ameanza dhidi ya England mjini Boston baada ya Marekani kumpatia visa ya kuingia nchini humo.