Norwich City yarudi tena Ligi Kuu England

LONDON, ENGLAND. NORWICH City imerejea Ligi Kuu England ikiwa imetumikia msimu mmoja tu kwenye Championship baada ya kushuka msimu uliopita wa 2019-20.
Miamba hiyo maarufu kwa jina la The Canaries imethibitisha kurejea kwenye Ligi Kuu England kwa msimu wa 2021-22 baada ya Swansea kushindwa kuifunga Wycombe nyumbani na Brentford kutoka suluhu na Millwall.
Swansea City ilitoka nyuma kwa mabao 2-0 kusawazisha mabao hayo mawili ndani ya dakika tatu, lakini walishindwa kupindua meza na kushinda mechi hiyo, huku Brentford walishindwa kupata ushindi mbele ya Millwall kwa kutoka sare ya bila ya kufungana, kitu ambacho kilikuwa habari njema kwa Norwich inayonolewa na kocha Mjerumani Daniel Farke.
Norwich ilishuka kutoka Ligi Kuu England msimu uliopita, lakini waliweka matumaini yao kwa kocha huyo Mjerumani na kubaki naye, ambaye kwa sasa amewarudisha kwenye ligi hiyo. Bado hawajaanza kusherehekea ubingwa wa Championship, lakini wanaongoza kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili, Watford. Na watapiga hatua kubwa kwenye kukaribia ubingwa wa Championship kama watakuwa wamewachapa Bournemouth kwenye mchezo uliopaswa kufanyika usiku wa Jumamosi uwanjani Carrow Road. Kama itakuwa imeshinda dhidi ya Bournemouth, basi Norwich watahitaji sare tu dhidi ya Watford Jumanne kutangazwa mabingwa wa ligi hiyo. Mechi zao tatu za mwisho msimu huu watacheza na QPR, Reading na Barnsley.
Norwich ilimaliza nafasi ya mwisho kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, ikiwa imevuna pointi 21 tu, ambapo ilishinda mechi tano tu. Hii ni mara ya nne kwenye kipindi cha miaka 10, Norwach City imekuwa ikishuka na kupanda Ligi Kuu England.