Ni usiku wa Ulaya, unaanzaje kulala!

Muktasari:

  • Rekodi mbovu ya Borussia Dortmund kwa mechi za ugenini na mambo matamu ya Real Madrid inapokuwa nyumbani ni kitu kinachozua mjadala katika mechi hizo wakati miamba hiyo itakapomenyana na Paris Saint-Germain na Bayern Munich mtawalia.

PARIS, UFARANSA: Kumekucha, zile mechi za marudiano za hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, zinapigwa wiki hii, ambapo leo Jumanne kipute kitakuwa huko Parc des Princes, wakati kesho Jumatano kasheshe lipo Santiago Bernabeu. Hakuna kulala.

Rekodi mbovu ya Borussia Dortmund kwa mechi za ugenini na mambo matamu ya Real Madrid inapokuwa nyumbani ni kitu kinachozua mjadala katika mechi hizo wakati miamba hiyo itakapomenyana na Paris Saint-Germain na Bayern Munich mtawalia.

PSG itakuwa nyumbani huko Paris kukipiga na Dortmund, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Signal Iduna Park, Jumatano iliyopita, lakini shughuli pevu itakuwa huko Bernabeu, ambapo Bayern itakwenda kukipiga na Real Madrid, ambayo kimsingi imekuwa na matokeo matamu sana inapocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani. Mechi ya kwanza iliisha kwa sare 2-2.

Katika mchezo wa kwanza, PSG haikuwa tu na bahati ya kufunga kwenye mechi ya kipigo cha bao 1-0 huko Dortmund, ambapo oligongesha mwamba mara mbili kupitia kwa Kylian Mbappe na Achraf Hakimi.

Kwa msimu huu, miamba hiyo ya Ufaransa imegongesha mwamba mara 10. Hivyo kwenye kipute cha marudiano, kocha Luis Enrique atahitaji wachezaji wake kuongeza umakini kwenye kutumbukiza mipira nyavuni. Mechi ya kwanza, PSG ilikuwa na wachezaji wengi vijana waliochuana na wale wenye uzoefu mkubwa kwenye kikosi cha Dortmund kama vile Mats Hummels, Emre Can, Marcel Sabitzer na Marco Reus. Safari hii itakuwaje?

Dortmund amekuwa na rekodi nzuri inapocheza nyumbani, ambapo haijapoteza kwenye mechi 11 zilizopita, ikishinda saba na sare nne.

Lakini, usiku wa leo watakuwa ugenini, mahali ambako kwenye mechi ya makundi walikubali kichapo cha mabao 2-0 walipocheza Parc des Princes. Na mbaya zaidi, katika mechi 11 za ugenini, imeshinda moja tu, sare moja na vichapo tisa.