Neymar? tulieni muone
Muktasari:
- Tetesi za Neymar kuondoka Al-Hilal zilianza kusambaa tangu wiki iliyopita ambapo ilielezwa Santos wamekubaliana na staa huyo kwamba atarudi kwenye timu hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 tangu aondoke.
RIYADH, SAUDI ARABIA: WAKALA wa staa wa Al-Hilal, Neymar Jr amekanusha uvumi kuhusu Mbrazi huyo kuondoka kwa matajiri hao wa Saudi Arabia na kurudi Santos.
Tetesi za Neymar kuondoka Al-Hilal zilianza kusambaa tangu wiki iliyopita ambapo ilielezwa Santos wamekubaliana na staa huyo kwamba atarudi kwenye timu hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 tangu aondoke.
Neymar amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha tangu alipojiunga na Al-Hilal, hali inayosababisha vigogo wa Hilal kufikiria kuachana naye.
Akizungumza kuhusu uvumi huo, Pini Zahavi alisema: "Hakuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu Neymar kuondoka Al-Hilal. Yuko chini ya mkataba na anafurahia sana kuwa hapa. Baba yake Neymar na mimi ndio watu pekee tunaoweza kusema kuhusu mustakabali wake. Sijui uvumi huu umetoka wapi."
Hata hivyo mwandishi wa habari za usajili Cesar Luis Merlo, ambaye ndio alianzisha uvumi wa Neymar kurudi Santos, ameijibu taarifa hiyo ya Zahavi akisema kwamba muda utathibitisha ukweli juu ya taarifa yake.
Neymar ambaye alirejea uwanjani msimu huu baada ya kukaa nje kwa karibia mwaka mzima ameumia tena na hatokuwepo pia katika mchezo wao dhidi ya Al-Khaleej, Jumamosi ya wiki hii.
Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na tangu atue Saudi Arabia amecheza mechi saba za michuano yote na kufunga bao moja tu.
Timu nyingine kutoka Brazil ambayo anahusishwa nayo ni Palmeiras lakini rais wao Leila Pereira ambaye alisema timu hiyo haiwezi kumsajili Neymar kwa sababu wao sio madaktari.
"Neymar hatojiunga Palmeiras, hii ni timu ya mpira na sio sehemu ya kutibia watu , nahitaji mtu ambaye atajiunga na kucheza muda huo huo, siwezi kukubali kusaini mchezaji ambaye hayupo sawa kimwili."