Neymar apata jeraha, aanza matibabu Santos
Muktasari:
- Uchunguzi wa kitabibu umeonesha kuwa Neymar ana uvimbe mdogo wa milimita mbili kwenye mguu wake wa kulia, jeraha lililotokea wakati wa mchezo ambao Santos ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Coritiba mwishoni mwa wiki iliyopita.
MSHAMBULIAJI wa Brazil, Neymar, amepata jeraha la misuli ya 'kiazi cha mguu' (calf injury) litakalomfanya akose mechi zijazo za klabu anayoitumikia ya Santos.
Hata hivyo, mkuu wa idara ya matibabu wa Santos, Rodrigo Zogaib, amethibitisha kuwa jeraha hilo si kubwa na mchezaji huyo atakuwa fiti ifikapo Mei 27, 2026 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya Kombe la Dunia 2026 na timu ya taifa ya Brazil.
Uchunguzi wa kitabibu umeonesha kuwa Neymar ana uvimbe mdogo wa milimita mbili kwenye mguu wake wa kulia, jeraha lililotokea wakati wa mchezo ambao Santos ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Coritiba mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kwa sasa, mchezaji huyo anapata matibabu maalum katika kituo cha mazoezi cha Santos chini ya uangalizi wa madaktari wake binafsi na wale wa Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) ili kuhakikisha anarejea uwanjani haraka iwezekanavyo.
Habari za jeraha hili zimeleta wasiwasi kwenye benchi la ufundi la timu ya taifa ya Brazil linaloongozwa na kocha Carlo Ancelotti, hasa ikizingatiwa kuwa Neymar alikuwa amejumuishwa kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 26.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Neymar kurejea timu ya taifa tangu Oktoba 2023, kwani Ancelotti amekuwa akisisitiza kuwaita wachezaji wenye utayari wa asilimia mia moja.
Licha ya changamoto hiyo, timu hiyo inatarajia kuwa Neymar atawahi mchezo wa kirafiki dhidi ya Panama uliopangwa kupigwa Mei 31, 2026.