Navas kumfuata Messi Miami
Muktasari:
- Navas aliyeichezea Real Madrid akiwa kipa enzi hizo Messi akikichezea kikosi cha Barcelona huko Hispania, kwa sasa anaichezea Pumas UNAM ya Mexico na amekuwa akizungumzia mara kwa mara mpango wake wa kwenda kucheza na Messi huko Marekan
NICOSIA, CYPRUS: STAA wa zamani wa Real Madrid, Keylor Navas anaweza kujiunga na Lionel Messi katika kikosi cha Inter Miami kinachoshiriki Ligi Kuu Marekani maarufu Major League mwishoni mwa msimu huu.
Navas aliyeichezea Real Madrid akiwa kipa enzi hizo Messi akikichezea kikosi cha Barcelona huko Hispania, kwa sasa anaichezea Pumas UNAM ya Mexico na amekuwa akizungumzia mara kwa mara mpango wake wa kwenda kucheza na Messi huko Marekani.
Navas hajaridhishwa na ofa ya kuongeza mkataba aliyopewa Pumas jambo ambalo limerahisisha mmiliki mwenza wa Inter Miami, David Beckham kumnyakua ifikapo mwishoni mwa msimu. Kipa huyo wa kimataifa wa Costa Rica anaonekana kuwa njiani kuondoka Pumas UNAM na huenda akajiunga na Inter Miami ambako amewekewa mkwanja wa maana mezani na Beckham ili asaini dili la kuitumikia timu hiyo kwa misimu mitatu.
Ofa ya kwanza ya Pumas ilikataliwa moja kwa moja na kipa huyo ambaye pia hajaridhishwa na ongezeko la mshahara pamoja na muda wa mkataba mpya wa mwaka mmoja badala ya miwili.
Kocha mkuu wa Pumas UNAM, Efrain Juarez anapambana kwa sasa kumshawishi mmiliki wa timu hiyo, Antonio Sancho kufanya juhudi za kifedha ili kumzuia kipa huyo kuondoka. Kwa upande wake, Navas vilevile anavutiwa na wazo la kumalizia maisha yake ya soka akicheza pamoja na Messi, akilenga kushinda mataji zaidi akiwa na timu hiyo ya Florida.
Changamoto pekee inayoonekana ni upande wa familia, kwani imezoea maisha ya Mexico, na kufanya uamuzi wa kuhama kuingiwa na sintofahamu, licha ya kwamba Miami ni mji wenye mvuto, hali nzuri ya hewa na mazingira ya Kilatino. Hata hivyo, Beckham ana nia ya kumsajili kipa mwenye jina kubwa kama Navas ili kumuongeza kwenye kikosi chake chenye nyota wengi.