Napoli yaweka mzigo kwa Darwin Nunez

Muktasari:
- Timu hiyo inamtaka mchezaji huyo katika dirisha hili la usajili wa majira kiangazi ikipambana kuweka sawa safu yake ya ushambuliaji inayomtegemea Romelu Lukaku kwa sasa
INAELEZWA kwamba Napoli imewasilisha ofa ya Pauni 42 milioni kwenda Liverpool kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Darwin Nunez, mwenye umri wa miaka 26.
Timu hiyo inamtaka mchezaji huyo katika dirisha hili la usajili wa majira kiangazi ikipambana kuweka sawa safu yake ya ushambuliaji inayomtegemea Romelu Lukaku kwa sasa
Hata hivyo, pale anakosekana mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mambo huwa magumu kikosini na ndio maana kwa sasa Napoli imeamua kupambana kuliweka sawa eneo la mbele la kusaka mabao.
Nunez ni miongoni mwa mastaa ambao Liverpool ipo tayari kuwauza katika dirisha hili la usajili kwani inadaiwa kwamba kocha Arne Slot havutiwi na utendaji wake wa kazi uwanjani.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, ambapo msimu uliomalizika alicheza mechi 47 za michuano yote na kufunga mabao saba.
Kwa upande wake Liverpool ipo kwenye mpango wa kutafuta mshambuliaji mpya ambaye ataziba pengo lakini hadi sasa hakuna iliyefamnikiwa kukamilisha usajili wake.
Mbali ya kiasi hicho cha pesa, Napoli pia imepanga kumpa Nunez mshahara kati ya euro 5 hadi 6 milioni kwa mwaka.
Ikiwa Liverpool haitokubalia kiasi hicho cha pesa ripoti kutoka Italia zinaeleza kuwa Napoli inaweza kumgeukia staa wa Udinese, Lorenzo Lucca ambaye inaweza kumnunua kwa Euro 34 milioni.
Eberechi Eze
ARSENAL iko tayari kumtoa mchezaji wake mmoja kama sehemu ya mabadilishano ili kuipata saini ya kiungo wa kati wa Crystal Palace, Eberechi Eze mwenye umri wa miaka 27, katika dirisha hili. Mbali ya Arsenal, huduma ya staa huyo pia inawindwa na vigogo mbalimbali barani Ulaya ikiwemo Tottenham Hotspur lakini inadaiwa Eze mwenyewe anataka kutua Arsenal.
Johan Bakayoko
VIGOGO wa Nottingham Forest wapo katika mazungumzo na wawakilishi wa winga wa PSV Eindhoven na timu ya taifa ya Ubelgiji, Johan Bakayoko mwenye umri wa miaka 22, kama mbadala wa Anthony Elanga, 23 aanayewindwa na Newcastle United. Bakayoko ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Nottingham Forest.
Anthony Elanga
MANCHESTER United inatarajiwa kupata Pauni 8 milioni ikiwa Nottingham Forest itamuuza Anthony Elanga kwenda Newcastle United katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Kiasi hicho cha pesa ni sehemu ya makubaliano ambayo Man United iliyaweka na vigogo wa Nottingham Forest 2023 wakati wa mauzo ya nyota huyo.
Malick Fofana
NOTTINGHAM Forest inaitaka saini ya winga wa Olympique Lyon na timu ya taifa ya Ubelgiji, Malick Fofana, 20, katika dirisha hili lakini inakumbana na upinzani mkali kutoka Chelsea na Bayern Munich ambazo zipo kwenye mazungumzo na wakala wake. Msimu uliopita Malick alicheza mechi 41 za michuano yote na kufunga mabao 11.
Leonardo Balerdi
NNEWCASTLE United inachunguza uwezekano wa kumsajili beki wa kati wa Marseille na timu ya taifa ya Argentina, Leonardo Balerdi, 26, ambaye pia anawindwa na Juventus. Balerdi ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Marseille na msimu uliopita alicheza mechi 29 za michuano yote. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika ifikapo 2028.
Cristhian Mosquera
JARIBIO la Arsenal la kutaka kumsajili beki wa Valencia na timu ya taifa ya Hispania, Cristhian Mosquera, 21, limekwama baada ya timu hiyo ya La Liga kuhitaji zaidi ya Pauni 20 milioni kama ada ya uhamisho. Mosquera ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Valencia na msimu uliomalizika amecheza mechi 41 za michuano yote.
Ferran Torres
KOCHA wa Aston Villa, Unai Emery amependekeza jina la mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Ferran Torres mwenye miaka 25, na anataka asajiliwe katika dirisha hili. Taarifa zinadai kwamba Villa ipo tayari kutoa kiasi kisichopunga Pauni 43 milioni kwa ajili ya kuipata saini yake kiasi ambacho kinaonekana kuwa kizuri kwa Barca.