Napoli yatimua kocha kabla ya kuivaa Barcelona

Muktasari:

  • Bosi wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, ameamua kumtimua Mazzarri baada ya timu yake kutoka sare juzi dhidi ya Genoa, lakini akiwa ana hofu kocha huyo hawezi kufanya vizuri kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho.

Napoli, Italia.  Klabu ya Napoli imetangaza kuachana na kocha wake wa muda Walter Mazzarri na kumpa timu hiyo Francesco Calzona, ambaye ataisimamia hadi mwishoni mwa msimu huu.

Awali Calzona alikuwa kocha msaidizi wa Maurizio Sarri na Luciano Spalletti kwenye kikosi cha Napoli, kabla hajaanza kusimama mwenyewe mwaka 2022, alipopewa nafasi ya kuifundisha timu ya taifa ya Slovakia.

Kocha huyo ameingia kwenye timu hiyo, ikiwa inajiandaa na mchezo wa hatua ya 16 bora wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona kesho kwenye Uwanja wa Maradona.

Calzona amesaini mkataba mfupi na Napoli hadi Juni 2024, pia ataendelea kuwa kocha wa timu hiyo ya taifa mpaka mwishoni mwa msimu huu.

Bosi wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, ameamua kumtimua Mazzarri baada ya timu yake kutoka sare juzi dhidi ya Genoa, lakini akiwa ana hofu kocha huyo hawezi kufanya vizuri kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho.

Baada ya kutwaa ubingwa wa Italia, msimu uliopita ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kupita miaka 30, timu hiyo imepita kwenye majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na  aliyekuwa kocha wake mkuu Luciano Spalletti na mkurugenzi wa ufundi Cristiano Giuntoli, kuachana na timu hiyo.

De Laurentiis alimchukua kocha wa zamani wa Al-Nassr Rudi Garcia, lakini mambo bado hayakwenda vizuri na Mfaransa huyo akatimuliwa mwishoni mwa mwaka jana, Mazzarri alipewa timu lakini mambo yakaendelea kuwa mabaya zaidi baada ya kuisimamia kwenye michezo 17, timu yake ilishinda michezo sita tu.

Lakini mbaya zaidi Napoli ilifunga mabao 16, katika michezo tisa kati ya hiyo  haikufunga bao lolote.

Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo ikiwa pointi tisa nyuma ya zile zilizopo nafasi ya nne.
Moja ya jukumu ambalo Calzona amepewa ni kuhakikisha Napoli inafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.