Mzigo wa usajili EPL ni kufuru
Muktasari:
- Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na FIFA kupitia wataalamu wake huko Zurich, Uswiss, klabu hizo zimetumia Pauni 2.38 bilioni kati ya jumla ya Pauni 7.28 bilioni zilizotumika katika dirisha la usajili lililofunguliwa kuanzia Juni 01 na kufungwa Jumatatu.
LONDON, ENGLAND: KLABU za Ligi Kuu England zimetumia karibu theluthi moja ya matumizi yote ya kimataifa ya usajili wa wachezaji dirisha hili la majira ya kiangazi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na FIFA kupitia wataalamu wake huko Zurich, Uswiss, klabu hizo zimetumia Pauni 2.38 bilioni kati ya jumla ya Pauni 7.28 bilioni zilizotumika katika dirisha la usajili lililofunguliwa kuanzia Juni 01 na kufungwa Jumatatu.
Kutokana na taarifa hiyo, Fifa ilisema soko la soka la wanaume linaendelea kuweka rekodi ya matumizi ambayo hayajawahi kutokea hapo awali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya sajili 12,000 zimefanyika katika dirisha hilo duniani kote kwa upande wa wanaume na matumizi yamepanda kwa asilimia 50 tofauti na ilivyokuwa mwaka 2024.
Fifa ilisema: “England imeimarisha nafasi yake kama nchi iliyotumia pesa nyingi zaidi katika usajili dirisha lililopita.”
Kuhusu idadi ya usajili wa wachezaji waliongia, England, Ureno na Brazil zilikamata nafasi tatu za juu kwa kuwa na namba kubwa ya wachezaji waliosajiliwa.
Katika soka la wanawake zaidi ya wachezaji 1,100 walisajiliwa kwa timu mbalimbali na jumla ya Pauni 9.2 milioni zilitumika katika na theluthi moja ya kiasi hicho ililipwa na timu za Marekani, zikifuatiwa na Ujerumani na England.
Mkuu wa masuala ya kisheria wa Fifa, Emilio Garcia Silvero alisema: “Tumeona soko la usajili likiendelea kuimarika kuanzia soka la wanaume na wanawake.Ingawa inaonekana ni kawaida kwa soka la wanaume hususan ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya Kombe la Dunia. Kuongezeka kwa takwimu katika usajili wa wachezaji wa soka la wanawake ni jambo la kushangaza kwani linathibitisha ukuaji wa kasi wa mchezo huo katika ngazi ya klabu.”
Idadi kubwa ya usajili uliofanyika dirisha lililopita ilisababisha matumizi ya rekodi ya dunia kwa klabu.
EPL pia ndiyo ligi iliyoweka rekodi ya kuwa na wachezaji waliosajiliwa kwa gharama kubwa zaidi kuliko ligi nyingine yoyote.
Uhamisho wa dakika za mwisho wa Alexander Isak kutoka Newcastle kwenda Liverpool ulikuwa mkubwa zaidi dirisha hili akisajiliwa kwa Pauni 130 milioni, pia usajili mwingine ni ule wa Florian Wirtz wa Pauni 116 milioni kutoka Bayer Leverkusen.
Mchezaji mwingine aliyesajiliwa kwa bei ghali ni Hugo Ekitike kutoka Eintracht Frankfurt, kwenda Liverpool kwa Pauni 69 milioni.
Uhamisho wa Benjamin Sesko kwenda Manchester United kwa Pauni 66 milioni, unaoweza kufikia Pauni 74 milioni pamoja na nyongeza, ulikuwa usajili wa nne mkubwa zaidi.
Vilevile usajili watano mkubwa ni ule wa ule wa Bryan Mbeumo kutoka Brentford kwenda Old Trafford kwa Pauni 65 milioni.
Bundesliga na Serie A zilikuwa ligi za pili na tatu kwa matumizi makubwa zaidi.
Klabu za Ujerumani zilitumia jumla ya Pauni 730 milioni kuimarisha vikosi vyao, huku timu za Serie A zilitumia Pauni 706 milioni. Ligue 1 ilitumia Pauni 543 milioni, huku na La Liga ikifunga tano bora ilitumia Pauni 495 milioni katika usajili.