Mzigo anao Kane kipute cha Madrid

Muktasari:

  • Kane na chama lake la Bayern Munich lilisafiri hadi Hispania kwenye kurudiana na Los Blancos na katika mchezo wa kwanza uliofanyika uwanjani Allianz Arenal timu hizo zilifungana 2-2.

MADRID, HISPANIA: Straika Harry Kane anaamini atapenya na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kwenda kumaliza gundu la kukosa mataji wakati usiku wa leo Jumatano atakapokabiliana na Real Madrid katika mchezo wa nusu fainali ya mikikimikiki hiyo utakaofanyika uwanjani Bernabeu.

Kane na chama lake la Bayern Munich lilisafiri hadi Hispania kwenye kurudiana na Los Blancos na katika mchezo wa kwanza uliofanyika uwanjani Allianz Arenal timu hizo zilifungana 2-2.

Katika mchezo wa kwanza, Vinicius Junior alifunga mara mbili, wakati mabao ya Bayern yalifungwa na winga Leroy Sane na mkwaju wa penalti ya Kane.

Bayern matumaini yao ya kubeba taji msimu huu yamebaki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya pekee baada ya kuangukia pua kwenye Bundesliga, ambapo taji hilo limebebwa na Bayer Leverkusen.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bayern kumaliza msimu bila ya taji tangu msimu wa 2011/12, hivyo Ligi ya Mabingwa Ulaya ni taji pekee lililobaki ambalo watalipambania.

Thomas Tuchel, ambaye aliongoza Chelsea kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021, alishatangaza kuachana na Bayern mwishoni mwa msimu huu, hivyo anaamini ataondoka na kitu.

Lakini, Real Madrid, yenyewe inafahamu namna ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa sababu tayari imeshanyakua taji la La Liga wikiendi iliyopita, nguvu zote sasa zimehamia kwenye ubingwa wa Ulaya na watachuana kuwania taji lao la 15.

Real Madrid haijapoteza kwenye mechi 20 tangu mara ya mwisho ilipochapwa na Atletico Madrid kwenye Copa del Rey, Januari. Safari hii, kipa wao namba moja, Thibaut Courtois anatarajia kurejea golini baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.