Mwisho wa ubabe AS FAR, Sundowns CAF
Muktasari:
- AS FAR inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na rekodi nzuri ya nyumbani katika mashindano hayo ya Afrika. Tangu mwaka 2005, imecheza mechi 29 za nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa na kupoteza mara tatu pekee.
RABAT, MOROCCO: AS FAR Rabat itaikaribisha Mamelodi Sundowns katika mechi ya marudiano ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa Jumapili hii Mei 24, 2026 mjini Rabat nchini Morocco, huku wenyeji wakihitaji kufuta kipigo cha mabao 1-0 walichopata Pretoria, wikiendi iliyopita.
AS FAR inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na rekodi nzuri ya nyumbani katika mashindano hayo ya Afrika. Tangu mwaka 2005, imecheza mechi 29 za nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa na kupoteza mara tatu pekee.
Hali hiyo inawapa matumaini makubwa ya kufanya ‘comeback’ mbele ya mashabiki wao kwenye Dimba la Prince Moulay Abdellah.
Katika historia hiyo, wamewahi kufungwa 1-0 na CS Sfaxien mwaka 2006, kabla ya kupoteza tena dhidi ya Étoile du Sahel mwaka 2007 na 2023. Mbali na matokeo hayo, wameshinda 18 na sare nane, ikiwemo ya 1-1 dhidi ya Sundowns kwenye hatua ya makundi mwaka 2024.
Kocha wa AS FAR, Alexandre Santos, alisema kikosi chake kina imani kubwa ya kubadili matokeo hayo nyumbani.
“Jambo muhimu ni kwenda nyumbani tukiwa na imani ya kupata ushindi na kufunga mabao yatakayotupa ubingwa. Tuna mashabiki wetu na mtindo wetu wa kucheza, hivyo kila kitu kinawezekana,” alisema Santos.
Kwa upande mwingine, Sundowns inaelekea Morocco ikifahamu kuwa itakutana na mazingira magumu na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa AS FAR. Mabingwa hao wa Afrika Kusini walipata ushindi mwembamba wa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza kupitia bao la mlinzi wa kushoto, Aubrey Modiba.
Kocha wa Sundowns, Miguel Cardoso, alisema anatarajia mchezo wa ushindani lakini akaomba spirit ya mchezo itawale baada ya vurugu zilizotokea Pretoria kati ya baadhi ya mashabiki wa AS FAR na polisi wa Afrika Kusini.
Katika mchezo huo wa kwanza, Sundowns walitawala umiliki wa mpira kwa asilimia 71 lakini walishindwa kuongeza mabao zaidi kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya AS FAR.
Kiungo wa AS FAR, Abdelfettah Hadraf, ametuma onyo kali kwa Sundowns akisisitiza kuwa timu yao ipo tayari kupambana hadi mwisho mbele ya mashabiki wao.
“Fainali inashindaniwa ili kubebwa, si kuchezwa tu. Wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wote tupo tayari kwa vita hii,” alisema Hadraf.
Safari ya Sundowns kuelekea Morocco pia ilikumbwa na changamoto baada ya kucheleweshewa kibali cha kutua Rabat, jambo lililowafanya wakae kwa saa kadhaa katika Uwanja wa Ndege wa OR Tambo kabla ya kusafiri siku iliyofuata. Hata hivyo nahodha Themba Zwane alisema morali ya timu ipo juu huku wakisaka ubingwa wao wa pili wa Afrika tangu walipotwaa taji hilo mwaka 2016.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani na nje ya uwanja, huku Sundowns wakijiandaa kukabiliana na presha kali kutoka kwa mashabiki wa Morocco katika pambano litakaloamua bingwa mpya wa Afrika.