Mwenyekiti PSG: Baada ya Messi, Mbappe 'hana sababu' ya kuondoka
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo Mfaransa anatarajiwa kuungana na Neymar na Messi katika safu ya ushambuliaji ya PSG, lakini nyota huyo wa Argentina hatarajiwi kuonekana mwishoni mwa wiki hii wakati klabu hiyo itakapovaana na Strasbourg.
Paris, Ufaransa (AFP). Mwenyekiti wa Paris Saint-Germain (PSG), Nasser al-Khelaifi leo Jumatano amesema mshambuliaji Kylian Mbappe "hana sababu" ya kuiacha klabu hiyo baada ya kuwasili kwa Lionel Messi, ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili.
Mbappe yuko katika mwaka wake wa mwisho wa mkataba wake na amekuwa akihusishwa na mipango ya kuondoka PSG, huku Real Madrid ikionyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo aliyekuwemo katika kikosi cha Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia.
"Kylian ni mkazi wa Paris, ni mshindani sana. Alisema alitaka timu yenye ushindani," alisema Al-Khelaifi.
"Kwa sasa hakuna aliye na ushindani zaidi yetu. Hana sababu ya kufanya lolote jingine," zaidi ya kubakia, aliongeza.
Mwezi Mei, mshambuliaji huyo mwenye miaka 22 aliiambia Canal Plus kuwa anataka kuwa sehemu ambako "anaweza hasa kushinda, ambako kuna mpango mzito."
Mbappe bado hajasaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Parc des Princes, tofauti na Neymar, ambaye hivi karibuni alikubaliana mkataba ambao utambakiza PSG hadi mwaka 2025.
Soma zaidi:PSG yafanya kufuru usajili wa Messi
Mshambuliaji huyo Mfaransa anatarajiwa kuungana na Neymar na Messi katika safu ya ushambuliaji ya PSG, lakini nyota huyo wa Argentina hatarajiwi kuonekana mwishoni mwa wiki hii wakati klabu hiyo itakapovaana na Strasbourg.