Mwamba huyu hapa! Huyo Sabitzer aliyetua Man United, we mpe jezi tu

MANCHESTER, ENGLAND. MTU mmoja anacheza namba kibao uwanjani. Marcel  Sabitzer ushawahi kulisikia hilo jina? Hujawahi? Basi usikonde kama unafuatilia Ligi Kuu England utaanza kumwona kwenye uzi wa Manchester United ya Eric ten Hag huko Old Trafford.

Utajiuliza nani huyo Sabitzer? Lakini, kocha wa zamani wa Austria, Thomas Janeschitz amesema kiungo huyo fundi wa mpira mwenye ujuzi mwingi miguu na anakimbia balaa uwanjani.

Janeschitz alisema hivi: “Man United imesajili mchezaji mwenye ufundi mwingi na anakikimbia sana uwanjani.”

Kama hujui, Man United imemsajili Sabitzer mwezi uliopita kama kiungo mchezeshaji, lakini mchezaji huyo ana uwezo pia wa kucheza kama straika, ambapo alikuwa akitumika hivyo kwenye kikosi cha timu yaike ya taifa ya Austria kilichokuwa chini ya kocha Marcel Koller

Na kwenye kushambulia, Sabitzer, 28, ni balaa kubwa, alifunga mabao 27 na kuasisti mara 21 katika msimu wake wa mwisho wakati alipokuwa akicheza ligi ya kwao huko Austria.

Uzuri wa kuwa na huduma ya Sabitzer ni kwamba unaweza kumtumia kama kiungo mshambuliaji, mshambuliaji au kwenye Namba 10 na wakati mwingine anaweza kukupa huduma bora kabisa akiwa winga.

Msimu wake wa kwanza alipokuwa RB Leipzig, Sabitzer alitumika kama winga wa kulia chini ya kocha Ralph Hasenhuttl na aliendelea kutamba kwenye eneo hilo chini ya Ralf Rangnick na baadaye Julian Nagelsmann.

Nagelsmann baadaye alimnunua Sabitzer akakipige Bayern Munich kwa mkwanja wa Pauni 12 milioni, Agosti 2021 na hapo akamhamisha nafasi na kumtumia kiungo wa kati, huku akitumika pia kama beki wa kushoto katika kikosi hicho cha Allianz Arena msimu huu.

Sabitzer ni mchezaji anayemudu nafasi nyingi kwa umakini mkubwa ndani ya uwanja, kocha anachopaswa kufanya ni kumpa tu jezi tu.

Kutokana na kuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kuanza huko Allianz Arena, Sabitzer akatimkia zake Man United kwa mkopo katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa Januari, Erik ten Hag alimsajili kwa mkopo akachukue mikoba ya kiungo majeruhi Christian Eriksen aliyeumia kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Reading.

Eriksen alisajiliwa na Man United na iliaminika angecheza zaidi Namba 10 au Namba 8, lakini badala yake alichezeshwa chini kwenye safu ya kiungo katika kikosi hicho msimu huu.

Akizungumzia majukumu ya Eriksen ndani ya uwanja, kocha Ten Hag alisema: “Tumeamua kumchezesha chini kidogo kama Namba 6 au 8 kwa sababu ni eneo linalomfanya awe huru zaidi.

“Tulimwambia ni nafasi gani anazopaswa kuwapo, lakini jambo zuri naye amezoea kwa wepesi majukumu hayo. Siku zote anakupa mchezo mzuri.”

Janeschitz alimzungumzia Sabitzer kwanini kiungo huyo anafaa kwenda kuziba pengo la Eriksen, aliambia hivi Sky Sports: “Namfahamu siku nyingi kabla tangu nilipokuwa nikifundisha timu ya taifa. Lakini, nadhani eneo lake bora zaidi ndani ya uwanja ni akicheza nyuma ya washambuliaji, pengine Namba 8 au Namba 10.

“Ni mzuri sana kiufundi anapokuwa na mpira kwenye miguu yake, anafunga mabao na anapiga mashuti akiwa umbali wowote ule. Tatizo kubwa kwa wapinzani lipo anaposhambulia ni hatari sana na amekuwa hodari pia kwenye kukaba. Anakimbia sana.

“Naamini ubora wake ni akicheza Namba 8 au Namba 10 kwa sababu anapenda kuwa na mpira kwenye miguu yake na anapiga pasi matata kwelikweli. Anaweza kucheza nafasi nyingi tofauti ndani ya uwanja. Huo ni ubora wake mwingine. Lakini, jambo kubwa mara zote anapocheza, faida yake ni ule uwezo mubwa wa kusoma mchezo.”

Janeschitz anaamini Sabitzer kwa tabia zake za kutaka kushinda atakuwa na mchango mkubwa huko Old Trafford – huku ikielezwa kwamba anaweza kushawishi hali ya mambo ili aendelee kubaki kwenye kikosi hicho baada ya muda wake wa mkopo wa miezi sita kufika tamati.

“Hapendi kupoteza mechi, kitu ambacho ni kizuri kwa afya ya timu,” alisema Janeschitz na kuongeza.

“Wakati mara ya kwanza tulipokuwa pamoja timu ya taifa kulikuwa na wachezaji wakubwa kikosini, lakini baada ya muda tu yeye akawa kiongozi. Sambamba na David Alaba na Marko Arnautovic, alikuwa miongoni mwa viongozi mashupavu kwenye kikosi cha Austria.”

Sabitzer alianzishwa kwenye mechi 20 tu kati ya 54 alizochezea Bayern Munich, hivyo atakuwa mwenye furaha kubwa kama atapata muda wa kutosha wa kucheza kwenye kikosi cha Man United.

“Kwa hilo ndio maana nafikiri amefanya uamuzi mzuri,” alisema Janeschitz na kuongeza. “Alikuwa na wakati mgumu Bayern na hakupewa nafasi ya kucheza kama ilivyotarajiwa.

“Kutokana na majeruhi Manchester United, atapata dakika za kutosha za kucheza na hicho ndicho anachotaka. Nimesikia kocha anampenda, hivyo hilo ni jambo bora pande zote. Presha ni kubwa, lakini nina hakika kwa uwezo wake na ubora uwanjani, ataweza kukabiliana na changamoto mpya huko Old Trafford.”

Mechi zajazo Man United

-Februari 4 vs Crystal Palace (nyumbani)

-Februari 8 vs Leeds United (nyumbani)

-Februari 12 vs Leeds United (ugenini)

-Februari 16 vs Barcelona (ugenini)

-Februari 19 vs Leicester City (nyumbani)

-Februari 23 vs Barcelona (nyumbani)

-Februari 26 vs Brentford (nyumbani)