Mpo? Agomea ndoa kisa soka
Muktasari:
- Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 ameweka wazi kuwa hana mpango wa kuoa hadi atakapostaafu kucheza soka, akieleza kuwa kwa sasa mchezo huo ndio kipaumbele chake kikubwa kuliko kitu kingine.
LOS ANGELES, MAREKANI:WAKATI mastaa wengi duniani wakianzisha familia sambamba na ma isha ya soka, nahodha wa Korea Kusini, Son Heung-min ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutanguliza soka mbele ya kila kitu, hata ndoa.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 ameweka wazi kuwa hana mpango wa kuoa hadi atakapostaafu kucheza soka, akieleza kuwa kwa sasa mchezo huo ndio kipaumbele chake kikubwa kuliko kitu kingine.
Kauli hiyo sio mpya kwa Son, kwani aliwahi kuizungumza tangu alipokuwa akiichezea Tottenham Hotspur ya England, akieleza kuwa ushauri huo aliupata kutoka kwa baba yake, Son Woong-jung ambaye amekuwa mtu muhimu katika safari yake ya soka la kulipwa.
Kwa mujibu wa Son, baba yake alimweleza kuwa mwanaume anapoingia kwenye ndoa, familia inakuwa jambo la kwanza katika maisha yake na sio kazi.
"Baba yangu amesema sipaswi kuoa mpaka nistaafu na nakubaliana naye. Ukioa, jambo la kwanza litakuwa familia, mke na watoto, halafu ndipo soka," alisema Son.
Mshambuliaji huyo amesema anatamani kuhakikisha kuwa kipindi chote anachocheza katika kiwango cha juu cha ushindani, soka linaendelea kuwa jambo namba moja katika maisha yake.
Son anaamini maisha ya familia yanaweza kusubiri lakini muda wa kucheza soka katika kiwango cha juu ni mfupi na hauwezi kurejea ukishapita.
"Unapostaafu ukiwa na miaka 33 au 34 bado utakuwa na maisha marefu ya kuishi na familia yako lakini nafasi ya kucheza soka katika kiwango cha juu haiwezi kudumu milele," alisema.
Licha ya kuwa mmoja wa wachezaji maarufu zaidi barani Asia na duniani, Son ameendelea kuishi maisha ya faragha tofauti na mastaa wengi wa soka.
Kwa muda mrefu amekuwa akijiepusha na kuweka wazi maisha yake ya kimapenzi huku ripoti mbalimbali zikieleza kuwa hana mke wala uhusiano wa wazi unaojulikana.
Msimamo huo umeifanya kauli yake ya kutanguliza soka kabla ya ndoa kuonekana kuwa sehemu ya falsafa yake ya maisha na taaluma.
Kilichovutia zaidi ni kwamba licha ya kufikisha miaka 33, Son bado hajaanza kuzungumzia mwisho wa safari yake ya soka.
Hivi karibuni alizima tetesi za kustaafu baada ya Kombe la Dunia 2026, akisema bado anajiona ana uwezo wa kuendelea kucheza soka la ushindani katika kiwango cha juu kwa miaka kadhaa ijayo.