Moyes anarudi mzigoni Everton
Muktasari:
- Mazungumzo baina yake na wamiliki wapya wa klabu hiyo, The Friedkin Group yamekwenda sawa na hivyo Moyes amerudi mzigoni Everton.
LIVERPOOL, ENGLAND: DAVID Moyes ametangazwa kuwa kocha mpya wa Everton baada ya kufikia makubaliano ya kurudi kupiga kazi huko Goodison Park.
Mazungumzo baina yake na wamiliki wapya wa klabu hiyo, The Friedkin Group yamekwenda sawa na hivyo Moyes amerudi mzigoni Everton.
Moyes atakuwa na majukumu ya kuiongoza timu hiyo katika kubadili hali ya mambo msimu huu, akimalizia mechi za mwisho katika uwanja wa Goodison Park kabla ya kuhamia kwenye uwanja mpya wa Bramley Moore Dock msimu ujao.
Wakati ikisubiriwa kutangazwa, makubaliano yanaripotiwa kufikiwa wikiendi ili kumpa nafasi Moyes ya kuanza kazi kuandaa timu yake kabla ya mchezo ujao wa Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa utakaofanyika huko Goodison Park, Jumatano.
Moyes alisema: “Ni jambo jema kurudi hapa! Nilifurahia kwa miaka 11 hapa, hivyo sikukataa kabisa ofa ya kurudi kwenye hii klabu kubwa. Nafurahi kufanya kazi na The Friedkin Group na nasubiri kwa hamu kuijenga timu upya.”
Mwenyekiti Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Marc Watts alisema: “Tumefurahi David kuungana nasi akiwa na historia kubwa ya Everton. Kwa uzoefu wake wa zaidi ya muongo mmoja atatuweka kwenye mstari mzuri wa kumalizia msimu wetu wa mwisho Goodison Park na kwenda kwenye uwanja mpya.”
Moyes aliinoa Everton kati ya mwaka 2002 na 2013. Alishinda mechi 218 kati ya 518 na aliisaidia Everton kumaliza kwenye Top Four 2004-05.
Everton ilimaliza nafasi saba za juu mara nane katika kipindi cha misimu 11 ya Moyes aliyokuwa kwenye timu hiyo. Aliisaidia kufika fainali ya Kombe la FA mwaka 2009 na kwenda kupoteza kwenye fainali dhidi ya Chelsea.