Mourinho arejea Real Madrid, Perez akimwaga Sh453 bilioni za usajili
Muktasari:
- Perez ameshinda kwa asilimia 65 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Enrique Riquelme aliyepata asilimia 35, katika uchaguzi ulioshirikisha wapiga kura zaidi ya 33,000 jana Jumapili, Juni 7, 2026.
MADRID, HISPANIA: Jose Mourinho amerejea rasmi kuwa kocha mkuu wa Real Madrid baada ya Florentino Perez kushinda tena uchaguzi wa urais wa klabu hiyo.
Perez ameshinda kwa asilimia 65 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Enrique Riquelme aliyepata asilimia 35, katika uchaguzi ulioshirikisha wapiga kura zaidi ya 33,000 jana Jumapili, Juni 7, 2026.
Baada ya ushindi huo uliompa Perez miaka mitano mingine madarakani, Real Madrid sasa itakamilisha malipo ya Euro 15 milioni (takriban Sh45.38 bilioni) kwenda Benfica ili kuvunja mkataba wa Mourinho.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 63 amesaini mkataba wa miaka mitatu kurejea kwenye timu hiyo aliyoiacha miaka 13 iliyopita, huku nafasi yake katika kikosi cha Benfica ikitarajiwa kuchukuliwa na kocha wa Fulham, Marco Silva.
Ushindi wa Perez pia unakuja na ahadi ya mapinduzi makubwa ya usajili ndani ya kikosi hicho kuelekea msimu mpyaa ambapo amepanga kutoa ofa ya rekodi ya Euro 150 milioni (Sh453.78 bilioni) kesho Jumanne, Juni 9, 2026 kumsajili mchezaji mkubwa wa daraja la juu (Galactico). Ingawa amekataa kutaja jina, ripoti zinadai anamnyatia winga wa Bayern Munich, Michael Olise.
Wakati huohuo, Real Madrid tayari imewasajili mabeki Ibrahima Konate na Denzel Dumfries, huku wachezaji wakongwe kama Dani Carvajal, David Alaba na Dani Ceballos wakionyeshwa mlango wa kutokea ili kupisha damu mpya.
Mourinho anakabiliwa na kibarua kizito cha kurejesha nidhamu na utulivu kwenye chumba cha kubadilishia nguo ambacho kimevurugika kufuatia migogoro ya wachezaji msimu huu. Hali hiyo ilifikia kilele mwezi uliopita baada ya kiungo Federico Valverde kukimbizwa hospitalini kufuatia ugomvi na Aurelien Tchouameni, tukio lililofanya wote wawili wapigwe faini ya Euro 500,000 (takriban Sh1.51 bilioni) kila mmoja.
Zaidi ya hayo, kocha huyo mpya atalazimika kufanya mabadiliko makubwa kwenye idara ya tiba na maandalizi ya viungo ili kukabiliana na janga la majeraha yaliyoandama timu hiyo msimu uliopita, ambapo yalirekodiwa 58 na kusababisha mivutano mikubwa kati ya klabu na kocha wa zamani, Xabi Alonso.