Moto ulivyowaka kwenye dabi zilizopigwa wikiendi

ACHANA na kipute cha Yanga na Simba cha Kariakoo dabi kilichopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi iliyopita, dunia ya wapenda soka ilishuhudia dabi za kutosha kwa wikiendi iliyopita.

Mabao ya Stephane Aziz Ki, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti na lile la Joseph Guede yalitosha kuipa Yanga ushindi mtamu na wa pili kwa msimu huu dhidi ya mahasimu wao Simba kwenye Ligi Kuu Bara, mabao 2-1 huku Wekundu wa Msimbazi ilifunga bao lao la kujifariji kupitia kwa Freddy Kouablan.


Lakini, Jumapili kulikuwa na kasheshe jingine huko Kenya kweye Mashemeji dabi kiliwaka kwenye Uwanja wa Nyayo, wakati Gor Mahia ilipoichapa AFC Leopards 1-0, shukrani kwa bao la Austin Odhiambo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Kenya na hivyo kuwafanya Kogalo kujitanua kileleni kwa kukusanya pointi 57 katika mechi 27.

Leopards yenyewe imebaki na pointi 38 kwenye nafasi ya nane katika msimamo wa ligi hiyo ya Kenya.

Kwa Yanga, ushindi wao kwenye Kariakoo dabi, umewafanya pia kujikita kileleni kwa kukuwanya pointi 58 katika mechi 22, wakati Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa imekusanya pointi 46 katika mechi 21.

Kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, katika kipute cha Zambia Super League, kulikuwa na dabi matata, Power Dynamos ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Nkana. Kipigo kimeizuia Power Dynamos iliyopo kwenye nafasi ya tatu na pointi 48 kuifikia ZESCO United kwenye nafasi ya pili, ikiwa imekusanya pointi 51, huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 29. Red Arrows ndiyo vinara wa ligi hiyo, wakikusanya pointi 61 katika mechi 29.


Huko Hispania, kulikuwa na dabi maarufu kabisa ya El Clasico, ambapo Real Madrid ilikuwa nyumbani kukipiga na mahasimu wao Barcelona katika mchezo wa La Liga, Jumapili.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa Los Blancos kushinda 3-2, Barcelona ndio waliokuwa wa kwanza kufunga kupitia kwa Andreas Christensen, lakini Madrid ilisawazisha kupitia Vinicius Jr kwa mkwaju wa penalti. Vijana wa Xavi walifunga tena kupindi cha pili kupitia kwa Fermin Lopez, lakini jeshi la Carlo Ancelotti lilifunga mara mbili zaidi, kupitia kwa Lucas Vazquez na Jude Bellingham na hivyo kushinda mchezo huo na kuweka pengo la pointi kufikia 11 baina ya timu hizo mbili. Madrid sasa imekusanya pointi 81 katika mechi 32 ikijitanua kileleni, wakati Barca ina pointi 70 kwenye nafasi ya pili baada ya mechi 32.

Shughuli nyingine ya wikiendi ya dabi kali ilikuwa huko Argentina, kwenye ligi ya Argentine Primera Division, ambapo River Plate ikiwa nyumbani ilikubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa mahasimu wao wakuu Boca Juniors.

River Plate ilitangulia kufunga kupitia kwa Miguel Borja mapema tu, lakini Boca ilisawazisha kabla ya mapumziko kupitia kwa Miguel Merentiel, ambaye alifunga mara mbili katika mchezo huo, ambapo lilikuwa bao la tatu kwa timu yake katika mchezo huo baada ya la pili kufungwa na Edinson Cavani kwenye kipindi hicho cha pili. Kwenye dakika za majeruhi, River Plate ilifunga bao lake la pili kupitia kwa Paulo Diaz, huku kipute kikifanyika kwenye Uwanja wa Estadio Mario Kempes.

Dabi nyingine ilikuwa kwenye Ligi Kuu England, huko Selhurst Park, ambapo Crystal Palace ilikuwa mwenyeji wa West Ham United kwenye London dabi, ambapo Palace ilishusha kipigo kizito cha mabao 5-2.

Mabao ya washindi katika mechi hiyo yalifungwa na Michael Olise, Eberechi Eze, Emerson Palmieri (amejifunga) na Jean-Philippe Mateta, aliyefunga mara mbili, wakati yale mawili ya kujifariji yaliyofungwa na vijana wa David Moyes, yaliwekwa nyavuni na Michail Antonio na kipa Dean Henderson, aliyejifunga.