Man City, Maresca ni suala la muda
Muktasari:
- Mwezi mmoja baada ya Pep Guardiola kutangaza kuondoka City baada ya miaka 10 ya mafanikio makubwa, taarifa zinaeleza kuwa makubaliano ya kumleta Maresca mwenye umri wa miaka 46 yako katika hatua za mwisho.
Manchester City wanakaribia kumteua aliyekuwa kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, kuwa meneja wao mpya kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya kufikia makubaliano ya fidia na Chelsea.
Mwezi mmoja baada ya Pep Guardiola kutangaza kuondoka City baada ya miaka 10 ya mafanikio makubwa, taarifa zinaeleza kuwa makubaliano ya kumleta Maresca mwenye umri wa miaka 46 yako katika hatua za mwisho.
BBC Sport iliripoti tarehe 8 Juni kuwa City na Chelsea walikuwa kwenye mazungumzo kuhusu fidia, ambayo sasa inaelezwa kuwa ni zaidi ya pauni10 milioni.
Chelsea wanaamini wanastahili kulipwa fidia kwa sababu Maresca alikuwa bado ana mkataba hadi mwaka 2029 kabla ya kuondoka Januari, na klabu hiyo ilikuwa ikichunguza hatua za kisheria zinazowezekana.
Chaguo la kwanza la City
Maresca alitajwa mapema kuwa ndiye mgombea pekee aliyekuwa akitafutwa na City kwa jukumu gumu la kurithi nafasi ya Guardiola.
Wachezaji wa City ambao hawapo kwenye majukumu ya Kombe la Dunia wanatarajiwa kurejea mazoezini katikati ya Julai kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Hata hivyo, kuchelewa kwa tangazo rasmi la Maresca kumewaacha baadhi ya wachezaji wanaofikiria mustakabali wao klabuni bila uhakika, kwa kuwa bado hawajakutana na kocha mpya kwa mazungumzo.
Usajili unaendelea
Licha ya kutokuwepo kwa kocha mpya rasmi, shughuli za usajili zimeendelea nyuma ya pazia.
City tayari wamekataliwa ofa mbili walizowasilisha kwa ajili ya kiungo wa Nottingham Forest, Elliot Anderson, lakini wanatarajiwa kurejea na ofa nyingine.
Inaaminika kuwa usajili huo unafanyika kwa idhini ya Maresca huku City wakitafuta mbadala wa nahodha anayeondoka, Bernardo Silva.
Enzi mpya baada ya Guardiola
Mwandishi wa City Xtra, Freddie Pye, amesema kuchelewa kwa tangazo rasmi huenda hakujaleta madhara makubwa kwa sababu maandalizi ya msimu mpya bado hayajaanza kikamilifu.
Iwapo uteuzi huo utakamilika rasmi, Maresca ataanza moja ya kazi ngumu zaidi katika soka la kisasa: kurithi nafasi ya Guardiola, ambaye ameiongoza Manchester City kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa na mashindano mengine makubwa katika kipindi chake cha miaka 10 klabuni.