Michael Owen: Ten Hag afukuzwe

Muktasari:

  • Kocha huyo alishuhudia kikosi chake cha Man United kikichapwa na Crystal Palace 4-0 usiku wa juzi Jumatatu na kumfanya straika staafu wa miamba hiyo ya Old Trafford, Owen kusema sasa muda wa Ten Hag kuendelea kuwa kocha kwenye kikosi hicho, umefika kikomo.

MANCHESTER, ENGLAND: Michael Owen ameitaka Manchester United kumfuta kazi Erik ten Hag.

Kocha huyo alishuhudia kikosi chake cha Man United kikichapwa na Crystal Palace 4-0 usiku wa juzi Jumatatu na kumfanya straika staafu wa miamba hiyo ya Old Trafford, Owen kusema sasa muda wa Ten Hag kuendelea kuwa kocha kwenye kikosi hicho, umefika kikomo.

Staa wa Palace, Michael Olise alikuwa steringi wa mchezo kwa kufunga mabao mawili, wakati mabao mengine ya wababe hao wa London yalifungwa na Jean-Philippe Mateta na Tyrick Mitchell.

Owen, 44, aliyetazama mechi hiyo mwanzo mwisho sambamba na gwiji mwingine wa Man United, Paul Scholes wanaamini umefika muda wa mabosi wa timu hiyo kuchukua hatua, kumfuta kazi Ten Hag.

Owen alisema klabu hiyo kwa hali ilipo kwa sasa haipaswi kupoteza mechi yoyote hadi mwisho wa msimu ili isikose nafasi ya kucheza kwenye michuano ya Europe League msimu ujao.

Alisema: “Nimesema kwa muda mrefu kwamba Ten Hag si mtu sahihi kwenye kazi hii ya kuinoa Man United. Nimezungumza hilo siku nyingi sana. Hana uwezo, naamini hatakuwa kocha wa timu hiyo msimu ujao.

“Wana mechi ya fainali ya Kombe la FA na wana mechi chache zilizobaki ambazo zinaweza kuwapa nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Lakini, wakati hilo likiendelea ni lazima ufanya uamuzi.

“Hakuna ubishi watakwenda kupigika dhidi ya Manchester City. Watakwenda kuteseka sana. Na kwa kifupi tu, Arsenal wataenda kuwafanya vibaya Old Trafford.

“Newcastle itawapiga na sijui hata kama watawaweza pia Brighton. Sioni kama watapata chochote kwa mechi zilizobaki hadi mwisho wa msimu. Ona, timu ipo kwenye hali mbaya na mechi zimebaki nne tu. Nitashangaa kama bodi haitajaribu kufanya jambo kuweka mambo sawa juu ya hii kitu.

“Hawezi kuendelea kuwa kocha wa hii timu msimu ujao. Hana uwezo. Nimekuwa nikisema hilo kwa muda mrefu, hana uwezo wa kutosha wa kuwa kocha wa Manchester United.”

Gwiji, Scholes alikubaliana na Owen alisema naye ameanza kupata hisia hizo za kutaka Ten Hag afutwe kazi baada ya kukubali kipigo kizito kutoka kwa timu kama Palace na kuona kinachotokea sasa ni kama kilichomtokea Ole Gunnar Solskjaer kwenye mechi zake za mwishoni alipokuwa Man United.

Kocha Solskjaer alifutwa kazi kwenye kikosi cha Man United baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Watford, mwaka 2021.

Scholes aliongeza: “Hizi dalili ndio kama zile kwamba kuna ugumu mkubwa kuona akiendelea kubaki kwenye timu hadi msimu ujao. Hii mechi niliona kama ni msumali wa mwisho kwenye jeneza. Hakika.

“Kulikuwa na kitu kisichoeleweka kwenye timu. Timu ilikuwa haina jitihada yoyote uwanjani. Kwenda kucheza na timu kama Crystal Palace, nisieleweka vibaya, ni timu nzuri, lakini sio kwa kuifanya kama vile Man United, siyo timu ya kuifunga Man United 4-0.

“Nani wa kuja kuchukua nafasi yake? Nani ambaye yupo? Hakuna mtu. Lakini kutokana na Thomas Tuchel kusema ataachana na Bayern Munich, basi hakuna tatizo. Kwa kiwango kile cha Man United, unaona kabisa huu ni mwisho wa Ten Hag. Amefika mwisho. Nakumbuka Ole Gunnar kwenye mechi ya Watford ugenini, 4-1. Hiki ndicho kilichotokea. Nauona mwisho umefika.”

Magwiji hao wanaamini Ten Hag atafunguliwa mlango wa kutokea mapema na kwamba timu ikabidhiwe kwa kocha Steve McClaren hadi mwisho wa msimu.

Wanachosisitiza ni kwamba wanaamini Ten Hag kwa sasa hana kitu ambacho atafanya, hivyo wanaamini akipewa kocha huyo wa zamani wa England, kuna kitu anaweza kukifanya.

Owen alisema: “Tulicheza chini ya Steve. Alitufundisha. Ujuzi wake hauonekani kabisa kwenye timu ya Man United. Ni kocha mahiri, lakini hi Man United ya sasa inaonekana kama haina kocha vile. Hapana.”

Wanachoamini magwiji hao ni kwamba McClaren ni msaidizi wa kocha Ten Hag, lakini hapewi nafasi ya kutua ushauri wake wa kiufundi na ndio maana timu hiyo inacheza soka lisiloeleweka.