Messi ni Alfa na Omega wa soka? kutoka Rosario hadi kilele cha dunia
Muktasari:
- Lilikuwa jambo la kipekee kwa sababu sio kila siku mchezaji mwenye umri wa karibu miaka 39 (anamiaka 38 na siku 357) anafunga mabao matatu katika fainali kubwa zaidi za soka duniani.
USIKU wa kuamkia leo, Jumatano Juni 17, 2026, dunia imeshuhudia balaa lingine la Lionel Messi. Nahodha huyo wa Argentina, alifunga hat-trick yake ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia na kuiongoza Argentina kuichapa Algeria mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi J.
Lilikuwa jambo la kipekee kwa sababu sio kila siku mchezaji mwenye umri wa karibu miaka 39 (anamiaka 38 na siku 357) anafunga mabao matatu katika fainali kubwa zaidi za soka duniani.
Lakini kwa Messi, mambo ambayo huonekana hayawezekani kwa wengine mara nyingi ndiyo yanakuwa kawaida kwake.
Hat-trick hiyo imemfanya kuwa na mabao 16 katika historia ya Kombe la Dunia na kumfanya afungane na mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani, Miroslav Klose, kama wafungaji bora wa muda wote wa michuano hiyo.
REKODI YA KLOSE MIKONONI MEAKE
Kwa miaka mingi Miroslav Klose alikuwa amekaa kileleni akiwa na mabao 16 aliyofunga katika Kombe la Dunia kuanzia mwaka 2002 hadi 2014.
Wakati wengi walidhani rekodi hiyo ingekuwa vigumu kuvunjwa kutokana na ugumu wa kufunga mara kwa mara katika michuano hiyo, Messi ameifikia akiwa amecheza Kombe la Dunia sita tofauti.
Kilichobaki sasa ni bao moja tu.
Argentina bado ina mechi za hatua ya makundi dhidi ya Austria na Jordan.
Endapo Messi atafunga bao moja pekee katika mojawapo ya mechi hizo, atakuwa mfungaji bora wa muda wote wa Kombe la Dunia akiwa amefikisha mabao 17.
Iwapo Argentina itafika hatua za mtoano, nafasi ya kuongeza idadi hiyo itaendelea kuongezeka.
HAT TRICK ILIYOCHELEWA LAKINI YENYE THAMANI
Cha kushangaza, licha ya kucheza Kombe la Dunia tangu mwaka 2006, Messi alikuwa hajawahi kufunga hat-trick katika fainali za michuano hiyo.
Hat-trick dhidi ya Algeria ndiyo ya kwanza katika maisha yake ya Kombe la Dunia.
Hii inaonyesha namna ambavyo michuano hiyo imekuwa ngumu hata kwa mchezaji wa kiwango chake.
Hata hivyo, wakati alipopata nafasi hiyo, aliifanya kwa mtindo wa kipekee na kuandika historia nyingine mpya.
Pia amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia tangu Kylian Mbappe alipofanya hivyo katika fainali ya mwaka 2022 dhidi ya Argentina nchini Qatar.
MFALME WA REKODI ZA ARGENTINA
Messi tayari ni mchezaji mwenye mechi nyingi zaidi katika historia ya Argentina akiwa amecheza mechi 200 za kimataifa, akionesha uimara na ubora kwa zaidi ya miaka 18 kwenye timu ya taifa.
Pia ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Albiceleste akiwa na mabao 116, huku pia akiwa mchezaji mwenye pasi 62 za mabao, idadi inayoonyesha mchango wake mkubwa si tu katika kufunga bali pia kutengeneza mabao kwa wengine.
Katika Kombe la Dunia, hakuna Muarjentina mwingine aliyewahi kufikia viwango vya Messi.
Baada ya hat-trick dhidi ya Algeria, amefikisha mabao 16 katika historia ya Kombe la Dunia, akifungana kileleni na Klose huku pia akiwa amecheza mechi 27 za Kombe la Dunia, idadi ambayo ni rekodi mpya katika historia ya michuano hiyo.
Kwa miaka mingi Diego Maradona alichukuliwa kama kipimo cha ukuu wa soka la Argentina kutokana na mchango wake wa kihistoria mwaka 1986.
Hata hivyo, baada ya Messi kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2022 na sasa kuifikia rekodi ya mabao ya Klose pamoja na kuendelea kuvunja rekodi nyingine mwaka 2026, mjadala wa nani mkubwa zaidi kati yao wawili unaweza kuwa na sura nyingi ambapo takwimu na mafanikio ya muda mrefu sasa yanampa Messi nafasi ya juu katika historia ya Albiceleste.
SAFARI ILIYOANZIA BARCELONA
Messi alizaliwa Rosario, Argentina mwaka 1987. Akiwa mtoto aligundulika kuwa na tatizo la homoni za ukuaji ambalo familia yake haikuweza kumudu gharama za matibabu.
Ndipo Barcelona ilipoamua kumchukua akiwa na umri mdogo na kugharamia matibabu yake.
Uamuzi huo ukabadilisha historia ya soka.
Kutoka kijana mdogo mwenye ndoto nyingi, Messi hadi kuwa nyota mkubwa wa Barcelona ambapo alishinda mataji zaidi ya 30, yakiwemo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, La Liga na Kombe la Dunia la Klabu.
Katika kipindi hicho alifunga mamia ya mabao, akashinda Ballon d'Or saba akiwa Barcelona huku ya nane akiipata akiwa PSG na kuweka viwango vipya vya ubora wa kiufundi duniani.
VITA VYA MILELE NA RONALDO
Hakuna mjadala wa Messi unaokamilika bila kumtaja Cristiano Ronaldo. Kwa zaidi ya miaka 15, wawili hao walitawala soka la dunia kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Ronaldo alijijenga kupitia nguvu, kasi, uwezo wa kuruka na kufunga kwa miguu yote pamoja na kichwa.
Messi kwa upande wake alitawala kupitia ubunifu, pasi, uwezo wa kukokota mpira, maono ya mchezo na uwezo wa kutengeneza nafasi ambazo wengine hawazioni.
Kwa pamoja wamevunja karibu kila rekodi muhimu ya mabao katika soka. Wakati Ronaldo akiwa mfungaji bora zaidi katika historia ya soka la kimataifa kwa mabao 138 ya timu za taifa, Messi amekuwa akifanya yake kupitia ubora wa jumla wa mchezo, ubunifu na mafanikio ya timu.
Kinachofanya mjadala huu kuwa mgumu ni kwamba wote wawili walifanikiwa katika zama moja. Lakini ushindi wa Kombe la Dunia mwaka 2022 na sasa rekodi ya mabao ya Kombe la Dunia inayokaribia kuvunjwa, vimempa Messi silaha nyingine kubwa katika mjadala huo.
HUU NDIYO MWISHO WA SAFARI
Swali kubwa sasa ni kama Kombe la Dunia 2026 litakuwa la mwisho kwa Messi.
Kama ndivyo, basi anaondoka akiwa ameshinda karibu kila kitu kinachoweza kushindaniwa katika soka.
Kombe la Dunia, Copa America, Ligi ya Mabingwa Ulaya, mataji ya ligi, Ballon d'Or, Golden Ball ya Kombe la Dunia na rekodi nyingi za mabao.
Lakini jambo la kushangaza ni kwamba bado anaonekana kuwa na njaa ya mafanikio. Dhidi ya Algeria hakukuwa na dalili za mchezaji anayefikiria kustaafu.
Kulikuwa na dalili za mtu ambaye bado anaamini ana kazi moja zaidi ya kufanya.
Kazi hiyo ni kuvunja rekodi ya Klose na kusimama peke yake kileleni mwa wafungaji wa Kombe la Dunia.
ALFA NA OMEGA?
Katika Biblia, Alfa na Omega humaanisha mwanzo na mwisho.
Je, Messi ni Alfa na Omega wa soka?
Jibu linaweza kutofautiana kulingana na upande unaounga mkono katika mjadala wa Messi, Ronaldo, Pele au Maradona.
Lakini jambo moja halina mjadala, wakati historia ya soka la dunia itakapokuwa ikiandikwa miaka mingi ijayo, jina la Lionel Messi litakuwa miongoni mwa majina machache yatakayochukua sura nzima ya mchezo huo.
Na baada ya usiku wa Kansas City, inawezekana kabisa dunia inashuhudia kurasa za mwisho za hadithi ya mchezaji ambaye wengi wanamchukulia kuwa bora zaidi kuwahi kucheza soka.