Austria yaanza na ushindi Kombe la Dunia baada ya miaka 28
Muktasari:
- Romano Schmid alianza kuifungia Austria bao dakika ya 21 na kuipeleka hadi mapumziko timu hiyo ikiongoza kabla ya Jordan kujibu mapigo katika kipindi cha pili na kusawazisha bao hilo kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Ali Olwan dakika ya 50.
CARLIFORNIA, MAREKANI: TIMU ya taifa ya Austria imeanza vyema kampeni zake za Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Jordan, katika mechi ya kikosi hicho ya Kundi J, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Levi's, Santa Clara, California, Marekani.
Romano Schmid alianza kuifungia Austria bao dakika ya 21 na kuipeleka hadi mapumziko timu hiyo ikiongoza kabla ya Jordan kujibu mapigo katika kipindi cha pili na kusawazisha bao hilo kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Ali Olwan dakika ya 50.
Austria iliandika bao la pili baada ya beki wa Jordan, Yazan Al Arab kujifunga mwenyewe akiwa katika harakati za kuuokoa mpira wa kichwa dakika ya 76, huku, Marko Arnautovic akafunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti kunako dakika ya 90+12.
Bao la Romano Schmid wa Austria ni la kwanza kwa kikosi hicho katika fainali za Kombe la Dunia baada ya miaka 28, tangu mara ya mwisho timu hiyo iliposhiriki mwaka 1998, ambapo kabla ya hapo nyota wa mwisho kufunga alikuwa ni Ivica Vastic.
Ivica ndiye aliyekuwa mchezaji wa mwisho wa Austria kufunga bao katika Kombe la Dunia la mwaka 1998, lililofanyika huko Ufaransa ambapo aliifungia timu hiyo katika mechi ya makundi dhidi ya Chile iliyoisha sare ya bao 1-1, Juni 17, 1998.
Katika mechi hiyo ya Juni 17, 1998, Chile iliongoza kupata bao kupitia kwa Marcelo Salas dakika ya 70, lakini Vastic aliisawazishia Austria dakika ya 90+1 na kusababisha pambano hilo la hatua ya makundi kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kwa upande wa Ali Olwan amekuwa ni mchezaji wa kwanza wa Jordan kufunga bao katika michuano ya Kombe la Dunia, akiwa ni nguzo muhimili ya kikosi hicho tangu kilipoanza kushiriki kufuzu mwaka 1985 kwa ajili ya fainali za mwaka 1986, Mexico.
Kwa takribani miaka 40, Jordan ilijaribu kushiriki bila ya mafanikio japo ilikaribia kufuzu mwaka 2014 na kushindwa katika hatua ya mtoano, baada ya kikosi hicho kuchapwa na Uruguay mabao 5-0, katika mechi iliyopigwa Novemba 13, 2013.
Hata hivyo, Juni 5, 2025, ndio ilikuwa siku ya kihistoria kwa kikosi hicho baada ya kufuzu rasmi Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, baada ya kuifunga Oman mabao 3-0, huku Ali Olwan aliyefunga leo akifunga mabao yote kwa maana ya Hat-Trick.