Messi Marekani kama CR 7 Saudia
Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa na Chama cha Wachezaji wa MLS (MLSPA), ambacho kimechapisha mishahara ya wachezaji wote wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza mwaka huu, inaonyesha kuwa hadi Aprili 16, 2026, wastani wa mishahara ya wachezaji wa MLS ni Dola 688,816 milioni kwa mwaka.
WASHINTON, MAREKANI: NAHODHA wa Inter Miami ya Ligi Kuu Marekani (MLS), Lionel Messi ameendelea kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwa mwaka wa tatu mfululizo baada ya kupata ongezeko kubwa la kipato mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Chama cha Wachezaji wa MLS (MLSPA), ambacho kimechapisha mishahara ya wachezaji wote wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza mwaka huu, inaonyesha kuwa hadi Aprili 16, 2026, wastani wa mishahara ya wachezaji wa MLS ni Dola 688,816 milioni kwa mwaka.
Oktoba mwaka jana, Messi alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu kuendelea kuichezea Inter Miami utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2028, muda mfupi kabla ya kuiongoza timu hiyo kutwaa taji la kwanza la MLS.
Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 38 hivi sasa analipwa mshahara wa msingi wa Dola 25 milioni kwa mwaka huku jumla ya malipo yake yaliyohakikiwa yakifikia Dola 28.3 milioni pamoja na marupurupu.
Hilo ni ongezeko kubwa ukilinganisha na msimu uliopita ambapo alikuwa akipokea mshahara wa msingi wa Dola 12 milioni na malipo ya jumla ya Dola 20.4 milioni.
Hata hivyo, ripoti zinaeleza kuwa Messi hupokea fedha nyingi zaidi ya kiwango hicho rasmi cha MLS.
Mmiliki wa Inter Miami, Jorge Mas, alisema klabu hiyo humlipa Messi kati ya Dola 70 milioni hadi 80 milioni kwa mwaka, jambo linalomfanya kuwa mchezaji wa pili anayelipwa zaidi duniani nyuma ya Cristiano Ronaldo anayekadiriwa kuingiza Dola 230 milioni akiwa Al Nassr.
Mbali na mshahara wake, Messi pia hupata fedha kupitia makubaliano ya kibiashara yanayohusiana na MLS na kampuni ya Adidas pamoja na mgawo wa mapato kutoka Apple TV. Biashara hizo pamoja na mikataba mingine ya matangazo zilimfanya kuingiza takribani Dola 135 milioni mwaka jana, kiwango ambacho kinaaminika kuongezeka zaidi mwaka huu kutokana na nyongeza ya mshahara na mikataba ya matangazo kuelekea Kombe la Dunia 2026.
Kwa upande mwingine, nyota wa LAFC, Son Heung-min ndiye mchezaji wa pili anayelipwa zaidi MLS baada ya Messi, ambapo Mkorea Kusini huyo analipwa mshahara wa msingi wa Dola 10.3 milioni huku malipo yake ya jumla yakifikia Dola 11.1 milioni.
Kiungo wa Inter Miami, Rodrigo De Paul anashika nafasi ya tatu akiwa na mshahara wa msingi wa Dola 7.5 milioni na malipo ya jumla ya Dola 9.6 milioni.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa wachezaji 10 wanaolipwa zaidi MLS 2026 wanatoka katika klabu tisa tofauti.
Kwa mujibu wa MLSPA, malipo ya jumla yaliyohakikiwa yanajumuisha mshahara wa msingi pamoja na bonas zote za usajili na malipo mengine ya uhakika yaliyogawanywa katika muda wote wa mkataba wa mchezaji.
1. Lionel Messi (Inter Miami Dola 28.3 milioni)
2. Son Heung-min (LAFC Dola 11.1 milioni)
3. Rodrigo De Paul (Inter Miami Dola 9.6 milioni)
4. Miguel Almiron (Atlanta Utd Dola 7.8 milioni)
5. Hirving Lozano (San Diego Dola 9.3 milioni)
6. Emil Forsberg (New York Red Bulls Dola 6 milioni)
7. Sam Surridge (Nashville Dola 5.9 milioni)
8. Ricard Puig Marti (LA Galaxy Dola 5.7 milioni)
9. Thomas Muller (Vancouver Whitecaps Dola 5.1 milioni)
10. Jonathan Bamba (Chicago Fire Dola 5.9 milioni)