Messi ataka kubaki, Barcelona kumpa miaka 10

Muktasari:

SUPASTAA, Lionel Messi amewaambia Barcelona ataendelea kubaki Nou Camp hata baada ya msimu huu kumalizika, kwa mujibu wa taarifa za Hispania.

BARCELONA, HISPANIA. SUPASTAA, Lionel Messi amewaambia Barcelona ataendelea kubaki Nou Camp hata baada ya msimu huu kumalizika, kwa mujibu wa taarifa za Hispania.

Mkataba wa supastaa huyo wa Kiargentina huko Nou Camp utafika tamati mwisho wa msimu huu na bado hajasaini dili jipya kumfanya abaki jambo lililokuwa likizua hofu kwamba huenda akaamua kuachana na maisha ya timu hiyo kutimkia kwingineko. Manchester City na Paris Saint-Germain zimeripotiwa kusaka saini yake.

Baba yake Messi, Jorge, ambaye ndiye wakala wake alisafiri kutoka Argentina hadi Hispania kwenda kujadili hatima ya mwanaye na rais wa Barcelona, Joan Laporta.

Na sasa, mshindi huyo mara sita wa Ballon d’Or amedhamiria kubaki kwenye klabu hiyo, kwa mujibu wa televisheni moja ya Hispania ya TVE. Messi alimwambia Laporta kwamba anahitaji kufanya uwekezaji mkubwa kwenye kikosi ili kurudi kwenye makali huku yeye hawezi kukubali kuchezea timu ambayo haishindanii mataji.

Messi ambaye umri wake wa sasa ni miaka 33 aliyedumu kwenye klabu hiyo ya Catalan tangu mdogo, anataka Barcelona ifanye usajili kunasa mastaa wa maana dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ikiwamo huduma ya straika wa Borussia Dortmund, Erling Haaland.

Na sasa taarifa za Nou Camp ni kwamba Messi yupo kwenye hatua za mwisho za kufanya uamuzi, huku Barcelona ikidaiwa kumpa ofa ya mkataba wa miaka 10.

Barcelona wanataka kumpa miaka 10 ili kuepuka ambacho kilitaka kutokea dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana, ambapo mkali huyo alilazimisha kuachana na timu hiyo, lakini klabu ilihitaji ilipwe Pauni 625 milioni kumwaachia aondoke.

Laporta tangu aliporudi kwenye klabu hiyo amekuwa akifanya jitihada kubwa kuhakikisha Messi haondoki na hiyo ndiyo ilikuwa ahadi yake kwa wanachama katika kipindi cha kampeni.

Kwa mujibu wa Times, dili matata la mkataba lipo mezani baada ya mazungumzo ya Laporta na baba’ke Meesi. Dili hilo pia linampa Messi ofa ya kubaki Nou Camp kwa muda mfupi kama atataka iwe hivyo ili aende akamalizie maisha ya soka kwenye Ligi Kuu Marekani.

Ataruhusiwa kwenda Marekani, lakini wakati huo akiendelea kuwa balozi wa Barcelona kabla ya kukaribishwa kwenye timu kuja kuchukua nafasi za uongozi wa juu wakati atakapotundika daruga.

Ripoti zinadai kwamba Messi anataka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara nyingi ne, hivyo atakubali kupunguza mshahara wake ili kuipa unafuu timu hiyo kuwa na pesa za kusajili mastaa wa viwango vya dunia.

Barcelona kwa sasa ni klabu yenye bili kubwa zaidi ya mishahara duniani na supastaa Messi ndiye anayepokea mkwanja mrefu zaidi, Pauni 584,000 kwa wiki baada ya makato.

Swahiba wake ambaye kwa sasa anakipiga Atletico Madrid, Luis Suarez alisema kuhusu Messi alipozungumza na TV3: “Kama Messi ataniomba ushauri kama rafiki, nitamwambia simuoni kwenye timu yoyote ile nyingine zaidi ya Barcelona. Uamuzi ni wake. Kitu bora zaidi ni kama atachukua miaka mitatu, minne, mitano au sita ya mwisho kwenye timu ambayo inamfanya kuwa na furaha. Barca inafurahi kwamba anajitolea kwa kila kitu na hana namna ni lazima ajitolee kwa kila kitu kwa ajili ya Barca.”