Mchakamchaka EPL kuendelea leo
Muktasari:
- Kipute kingine cha moto kwa Jumatano, kitawashuhudia vinara Liverpool ambao watakuwa nyumbani Anfield kukipiga na Newcastle United. Ni balaa zito.
LONDON, ENGLAND: MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu England unaendelea Jumanne. Lakini, kitu kitamu ni Jumatano, kutakuwa na mechi za kibabe zaidi, ikiwamo Tottenham Hotspur na Manchester City huko London.
Kipute kingine cha moto kwa Jumatano, kitawashuhudia vinara Liverpool ambao watakuwa nyumbani Anfield kukipiga na Newcastle United. Ni balaa zito.
Jumatano itakuwa ya mechi nyingi za kibabe na Arsenal baada ya kukumbana na kipigo cha kushtua wikiendi iliyopita, itakwenda ugenini kukipiga na Nottingham Forest, ambayo imekuwa na kiwango bora sana msimu huu. Itakuwaje? Ngoja tuone.
Huko Old Trafford kutakuwa na mechi inayokutanisha timu mbili zitakazochuana kwenda vita ya kukataa kushuka daraja, ambapo Manchester United itaikaribisha Ipswich Town.
Mechi ya kwanza kwenye Ligi Kuu England baina ya timu hizo, ambayo ilikuwa ya kwanza kwa Kocha Ruben Amorim, timu hizo zilitoka sare. Safari hii itakuwaje?
Kasheshe jingine kwa Jumatano, litakuwa kwenye kipute kitakachokutanisha Brentford, ambao watakipiga na Everton iliyokuwa balaa kwa siku za karibuni tangu ilipoanza kuwa chini ya kocha David Moyes.
Kwa mechi za Jumanne, Brighton itakuwa nyumbani kukipiga na Bournemouth, wakati Crystal Palace itakuwa na shughuli pevu mbele ya vijana wa Unai Emery, Aston Villa katika moja ya mechi yenye upinzani mkali zitakazopigwa wiki hii.
Wolves itakuwa nyumbani kucheza na Fulham, sawa na Chelsea ambayo itajimwaga kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Stamford Bridge kukipiga na Southampton, ikijaribu kusaka ushindi wa kuwapoza mashabiki wao baada ya kukumbana na kipigo kwenye mechi iliyopita mbele ya Aston Villa.
Alhamisi kutakuwa na mchezo mmoja tu kwenye ligi hiyo na West Ham United itakaribisha Leicester City, ambayo imekuwa na matokeo ya hovyo katika mechi za karibuni ikiwa chini ya kocha Ruud van Nistelrooy.