Mbappe njiani kuvunja rekodi ya Ronaldo UCL
Muktasari:
- Mbappe aliipa Real Madrid matumaini kidogo katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich uliopigwa juzi, ambapo bao lake la thamani linaweza kuwa la uamuzi wanapoelekea Munich kwa mchezo wa marudiano wakiwa na nafasi nzuri ya kusonga mbele.
MADRID, HISPANIA: STRAIKA wa Real Madrid, Kylian Mbappe yupo karibu kiasi gani kuvunja rekodi ya mabao ya msimu mmoja ya Cristiano Ronaldo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mbappe aliipa Real Madrid matumaini kidogo katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich uliopigwa juzi, ambapo bao lake la thamani linaweza kuwa la uamuzi wanapoelekea Munich kwa mchezo wa marudiano wakiwa na nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Katika mchezo huo Real Madrid ililala kwa mabao 2-1 ikiwa nyumbani, ambapo bao la wababe wa Santiago Bernabeu lilifungwa na Mbappe huku Bayern Munich ikipata mabao yake kupitia kwa Luis Diaz na Harry Kane.
Bao hilo kwa Mbappe lilikuwa lake la 14 katika ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu akilingana na rekodi ya juu ya msimu mmoja aliyowahi kuiweka Lionel Messi katika maisha yake ya soka, na kumuacha Mbappe akiwa mabao matatu nyuma ya rekodi ya muda wote ya Cristiano Ronaldo.
Ronaldo alifikia mabao 14 au zaidi katika misimu mitatu tofauti, lakini rekodi yake binafsi bado ni mabao 17 aliyofunga msimu wa 2013/14. Hii ina maana Mbappe sasa anahitaji mabao matatu ili kufikia rekodi hiyo, ingawa itakuwa ngumu zaidi ikiwa Real Madrid haitafanikiwa kuipindua Bayern Munich katika mchezo wa marudiano.
Katika mchezo wa pili huko Munich, Mbappe atahitaji kufunga hat-trick ili kulingana na rekodi ya Ronaldo na hilo linaonekana kuwa gumu, hasa dhidi ya kipa Manuel Neuer ambaye alikuwa katika kiwango bora kabisa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.
Katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuna wachezaji wa soka saba ambao wamefikia kiwango cha kufunga mabao 14+ kwa msimu mmoja. Mbappe amekuwa mchezaji muhimu zaidi wa Real Madrid katika nyakati za muhimu.
Mwezi huu, Real Madrid inapambania mataji yote ya ndani na kimataifa na ikiwa itaaangushwa katika Ligi ya Mabingwa mtazamo utageukia kwenye mbio za LaLiga, ambapo kwa sasa iko nyuma ya Barcelona kwa tofauti ya pointi saba.
Lakini, hata kama itaondolewa Ligi ya Mabingwa wiki ijayo huko Ujerumani, msimu huu utaendelea kuwa wa kihistoria kwa Mbappe, lakini kumaliza bila taji na bila kuvunja rekodi kutatafsirika ni kushindwa kwa nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa.