Mbappe anga za wakubwa

Muktasari:

  • Mabao hayo mawili aliyofunga Nou Camp yamemfanya Mbappe, 25, kufikisha mabao 48 kwenye michuano hiyo na kulingana na magwiji wawili wa AC Milan, Andriy Shevchenko na Zlatan Ibrahimovic.

PARIS, UFARANSA: Supastaa, Kylian Mbappe ametinga kwenye 10 bora ya vinara wa muda wote wa mabao kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupiga mbili dhidi ya Barcelona na kulisaidia chama lake la Paris Saint-Germain kutinga nusu fainali ya michuano hiyo msimu huu kwa jumla ya mabao 6-4.


Mabao hayo mawili aliyofunga Nou Camp yamemfanya Mbappe, 25, kufikisha mabao 48 kwenye michuano hiyo na kulingana na magwiji wawili wa AC Milan, Andriy Shevchenko na Zlatan Ibrahimovic.


Hata hivyo, magwiji hao wawili walihitaji kucheza mechi walau 100 kufikisha idadi hiyo ya mabao 48, wakati Mbappe amefikisha baada ya mechi 71 tu, alizocheza akiwa na AS Monaco na PSG.


Na sasa fowadi huyo wa kimataifa wa Ufaransa ameingia kwenye 10 bora ya vinara wa muda wote wa mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiwa amebakiza bao moja tu kumfikia gwiji wa Real Madrid, Alfredo Di Stefano.


Hii hapa orodha kamili ya mastaa hao 10 wanaoongoza kwa mabao na mechi walizocheza kufikisha idadi hiyo ya mabao waliyofunga katika mikikimikiki hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu huko Ulaya.


Supastaa, Cristiano Ronaldo anaongoza baada ya kufunga mabao 140 katika mechi 183, alizocheza akiwa na Manchester United, Real Madrid na Juventus, akifuatiwa na supastaa mwingine, Lionel Messi alifunga mabao 129 katika mechi 163 alipozichezea Barcelona na PSG.


Staa anayekamilisha tatu bora ni straika wa Barcelona, Robert Lewandowski, aliyefunga mara 94 katika mechi 120, huku akifanya hivyo akiwa katika vikosi vya Borussia Dortmund, Bayern Munich na Barcelona.


Karim Benzema amefunga mabao 90 katika mechi 152 alizocheza Lyon na Real Madrid, wakati Raul alifunga mara 71 katika mechi 142 kwenye vikosi vya Real Madrid na Schalke 04, huku Ruud van Nistelrooy akifunga mabao 56 katika mechi 73 alizocheza PSV Eindhoven, Man United na Real Madrid, wakati Thomas Muller wa Bayern Munich kabla ya mechi ya usiku wa jana Jumatano dhidi ya Arsenal alikuwa amefunga mabao 54 katika mechi 149, wakati Thierry Henry alifunga mabao 50 katika mechi 112 akiwa na Monaco, Arsenal na Barcelona na gwiji wa Real Madrid, Alfredo Di Stefano alifunga 49 katika mechi 58 na Mbappe akikamilisha idadi hiyo kwa kufunga mabao 48 katika mechi 71.