Mbadala wa Saka ni huyu
Muktasari:
- Kuna uwezekano mkubwa washika mitutu hao wa Jiji la London wakasajili mshambuliaji kwa sababu Saka atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha aliyopata Jumamosi ya wiki iliyopita dhidi ya Crystal Palace.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL huenda ikamsajili mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Randal Kolo-Muani, katika dirisha lijalo kwa ajili ya kuziba pengo la staa wao Bukayo Saka.
Kuna uwezekano mkubwa washika mitutu hao wa Jiji la London wakasajili mshambuliaji kwa sababu Saka atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha aliyopata Jumamosi ya wiki iliyopita dhidi ya Crystal Palace.
Taarifa zinaeleza kuwa staa huyo anaweza kukosa mechi 15 kwani atakaa nje ya uwanja walau hadi Machi mwakani.
Ili kuziba pengo lake katika kipindi hicho, Arteta anadaiwa kutaka mshambuliaji na kwa sasa Kolo-Muani inaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kumpata.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, mwenye umri wa miaka 26, amekuwa akipata nafasi ndogo ya kucheza katika kikosi cha PSG na ameshaomba kuondoka Januari.
Kolo-Muani ameanza katika mechi mbili tu kwenye Ligue 1 msimu huu, licha ya kuhamia PSG kwa kitita cha Pauni 75 milioni kutoka Eintracht Frankfurt 2023.
Licha ya kucheza zaidi kama mshambuliaji wa kati, Kolo-Muani mara nyingi anaweza kucheza pia kama mshambuliaji wa pembeni, upande wa kushoto au kulia, na hii inamaanisha anaweza kuziba nafasi ya Saka ikiwa atasajiliwa Arsenal.
Awali, haikuonekana kama Arsenal itafikiria kusajili mshambuliaji anayetokea pembeni lakini majeraha waliyopata Saka na Raheem Sterling yamebadilisha upepo.
Hivi karibuni, kocha Mikel Arteta alisema anataka kuziba nafasi za Saka na Sterling kwa kuanza kutumia wachezaji wa ndani kama Gabriel Martinelli, Leandro Trossard, Gabriel Jesus na Ethan Nwaneri.
Hata hivyo, kocha huyu akaongeza kwamba ikiwa hatopata anachokihitaji basi wanaweza kuhamia nje kutafuta mbadala.