Mayele uso kwa uso na Osimhen
Muktasari:
- Mshindi wa mechi hiyo, atatinga hatua ya FIFA Inter-Continental Play-Off yenye timu sita mwezi Machi ambapo nafasi mbili zitatolewa kwa Kombe la Dunia huku aliyefungwa akifunga ukurasa wa safari ya 2026.
TIMU ya taifa la Nigeria na DR Congo zitamenyana Jumapili katika fainali ya mchujo wa CAF wa kufuzu Kombe la Dunia jijini Rabat, Morocco, ambapo mshindi atafuzu hatua ya FIFA Inter-Continental Play-Off Machi, 2026 na kuendeleza matumaini ya kushiriki Kombe la Dunia 2026.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja waPrince Héritier Moulay El Hassan.
Kikosi kinachonolewa na Eric Sékou Chelle, Super Eagles kitaingia katika mechi hiyo kikiwa na morali ya aina yake baada ya ushindi wa juzi Alhamisi wa mabao 4–1 kupitia dakika za nyongeza dhidi ya Gabon. Nigeria ililazimishwa sare mwishoni mwa muda wa kawaida, lakini ikafanya kweli katika dakika 30 za nyongeza.
Ni Chidera Ejuke aliyefungua karamu ya mabao mapema tu baada ya muda huo kuongezwa kabla ya Victor Osimhen kufunga mabao mawili na kuihakikishia miamba hiyo kutinga fainali ya mchujo. Awali Adams ndiye aliyefunga bao la kuongoza katika dakika ya 78 katika dakika 90 kabla ya Lemina kuchomoa kwa Gabon katika dakika ya 89.
Mabingwa hao mara tatu wa Afrika wamesaliwa na dakika 90 tu kucheza hatua ya pili ya mchujo wa dunia nzima, nafasi ambayo itatoa tiketi ya kumi kwa Afrika katika Kombe la Dunia 2026.
Upande wa pili, DR Congo iliingia fainali hii kwa tabu, ikipata ushindi mwembamba wa bao 1–0 dhidi ya Cameroon kupitia bao la dakika za nyongeza lililofungwa na nahodha Chancel Mbemba, aliyemalizia krosi ya kona ya Cipenga.
Kikosi hicho kinachonolewa na Sébastien Desabre kilikuwa bora katika kujilinda huku kipa wao, Lionel Mpasi akifanya kazi kubwa kwa kuokoa michomo ya hatari.
Fainali hii inatarajiwa kuwa na ushindi mkubwa kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili, Nigeria inajivunia ubora wa safu yao ya ushambuliaji ikiongozwa na Osimhen, DR Congo yenyewe inajivunia uwezo wake wa kulinda huku wakisifika kuwa na ubora wa kutumia mipira ya adhabu.
Uzoefu wa Cédric Bakambu na makali ya nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele zinaipa DR Congo nafasi ya kuangusha mbuyu Nigeria.
Mshindi wa mechi hiyo, atatinga hatua ya FIFA Inter-Continental Play-Off yenye timu sita mwezi Machi ambapo nafasi mbili zitatolewa kwa Kombe la Dunia huku aliyefungwa akifunga ukurasa wa safari ya 2026.
Kama timu moja kati ya DR Congo na Nigeria zitaungana na wawakilishi tisa wa Afrika waliofuzu moja kwa moja fainali hizo zitakazofanyikia katika nchi za Marekani, Canada na Mexico ambazo ni Morocco, Tunisia, Algeria, Misri, Ghana, Afrika Kusini, Senegal, Cape Verde na Ivory Coast.