Mastaa hawa wanatajirika bila jasho EPL

LONDON, ENGLAND. LIGI KUU England imeendelea kupamba moto ikiwa imefikia mzunguko wa 12, hadi sasa kuna mastaa waliong’aa kwenye ufungaji wa mabao, wengine wameng’aa kwenye utoaji wa pasi za mabao na wengine wameng’aa kwenye upigaji wa pasi zilizofika.

Takwimu ni nyingi na kila mchezaji anatamba kwenye eneo lake bila kusahau makipa ambao wanatamba kupitia kuokoa michomo na kumaliza mechi bila ya kuruhusu bao.

Sasa wakati hawa wanajisifia kwa takwimu nzuri kuna kundi la wachezaji ambao wao wanajikunjia pesa bila ya kufanya kazi yoyote kwani baadhi yao hawajacheza mechi hata moja ya Ligi Kuu England ama michuano yoyote na wengine wamecheza mechi za michuano mingine lakini hawajacheza kwenye EPL. Hii hapa ni orodha ya mastaa ambao wametulia tu benchini wamekunja nne, lakini wanapata pesa nyingi balaa.

DONNY VAN DE BEEK

Mbali ya majeraha ya mara kwa mara yanayomsumbua bado pale anapokuwa amepona huwa hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Man United.

Awali, ilidhaniwa kuwa huenda angepewa muda mwingi wa kucheza kutokana na ujio wa Erik Ten Hag kwenye kikosi cha mashetani wekundu hao lakini mambo yamekuwa ni tofauti.

Staa huyu raia wa Uholanzi analipwa Pauni 120,000 kwa wiki na hadi sasa amevuna Pauni 1.68 milioni kutokana na mshahara huku akiwa amecheza mechi mbili tu ambazo zote ameingia akitokea benchini na ukijumlisha dakika alizocheza ni 21 tu. Kwenye EPL amecheza mechi moja dhidi ya Crystal Palace ambayo ametumika dakika mbili.


CLEMENT LENGLET

Beki wa kati huyu ambaye amejiunga na Aston Villa kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Barcelona ni mmoja kati ya mastaa watatu wanaovuta mkwanja mrefu kwenye kikosi cha Villa, akijipatia Pauni 150,000 kwa wiki.

Pesa hizo zote zinatoka kwenye mfuko wa Villa lakini alichowapa hadi sasa ni tofauti na matarajio, kwani tangu msimu uanze amecheza mechi nne tu ambazo zote ni za Uefa Conference League na kwenye Ligi Kuu England hajacheza hata mechi moja tangu msimu uanze. Hadi sasa Villa imeshamlipa Pauni 2.1 milioni.


HUGO LlORIS

Karibia mechi zote 12 kwa msimu huu pale langoni kwa Tottenham amesimama Guglielmo Vicario, Nafasi ya Lloris haionekani kuwepo mbele ya kocha Ange Postecoglou.

Lakini kutokucheza kwake kunaipa hasara sana Spurs ambayo inamlipa Pauni 100,000 kwa wiki na kufikia sasa hajacheza hata mechi moja.

Hadi sasa Spurs imemlipa kiasi kisichopungua Pauni 1 milioni ambayo hajaitumikia uwanjani hata kwa dakika moja.


FRASER FORSTER

Huyu naye ni kipa anayekalishwa benchi na Guglielmo Vicario pale Spurs, lakini walau huyu ameitumikia pesa anayoipata kwenye mechi moja.

Kipa huyu raia wa England kwa wiki anakunja Pauni 75,000, licha ya kwamba hajacheza hata mechi moja ya Ligi Kuu England amewahi kuitumikia Tottenham kwenye michuano ya Carabao dhidi ya Fulham na akashindwa kutetea lango lake na Spurs ikapoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti. Hadi sasa amevuna Pauni 1 milioni.


CEDRIC SOARES

Beki huyu wa kulia haonekani kuwa na nafasi mbele ya Ben White na Tomiyasu, kwenye kikosi cha washika mitutu. Lakini haimfanyi yeye kushindwa kukunja mkwanja wa kutosha.

Inaelezwa kuwa  analipwa Pauni 75,000 kwa wiki na hadi sasa amepata kiasi kisichopungua Pauni 1.05 milioni, lakini huyu pia ametumikia mshahara wake kidogo kwa kucheza mechi mbili za michuano ya Carabao ingawa ukijumlisha mechi zote hizo amecheza dakika 72 tu.


BEN GODFREY

Wakati huu ambao timu inaonekana kutofanya vizuri, kocha Sean Dyche haonekani kabisa kumuamini, staa huyu raia wa England ambaye alijiunga na Everton mwaka 2020 akitokea Norway ambaye kiujumla analipwa Pauni 75,000 kwa wiki. Hadi sasa amecheza mechi moja tu kwenye Ligi Kuu England na moja kwenye Carabao. Kwenye EPL amecheza dakika moja tu.

Everton imeshatoa Pauni 1.05 milioni kumlipa staa huyu kama mshahara na takwimu ndani ya dakika moja aliyocheza kwenye EPL ameitumikia kwa Pauni 1.05 milioni.


LUKASZ FABIANSKI

Amekuwa chini ya Alphonse Areola tangu msimu uliopita. Kipa huyu raia wa Poland analipwa Pauni 65,000 kwa wiki na hadi sasa amekusanya mkwanja usiopungua Pauni 910,000.

Hajaichezea West Ham hata mechi moja kwa upande wa Ligi Kuu England lakini kwenye upande wa Ulaya amecheza mechi tatu na Kombe la Ligi (Carabao) amecheza mechi mbili.MAXIWEL CORNET

Huyu pia amecheza mechi tano za michuano yote, ambazo kwenye EPL amecheza moja tu. Winga huyu wa kushoto kwa wiki anapewa Pauni 65,000 na hadi sasa amepata kiasi kisichopungua Pauni 910,000.

Kwenye mechi hizo tano alizocheza nyingi aliingia akitokea benchini na upande wa EPL alikocheza mechi moja alitumia dakika moja tu.

Staa huyu ni mmoja ya wachezaji waliosajiliwa kwa  matumaini makubwa akitokea Burnley mwaka jana lakini ameshindwa kumshawishi David Moyes.

ADRIAN

Imekuwa ngumu kwake kupenya mbele ya Alisson Becker, hivyo hajacheza hata mechi moja ya kusingiziwa lakini hiyo haimzuii kuendelea kujipatia pesa akiwa anaangalia wenzake wanacheza.

Jamaa kwa wiki anapata Pauni 60,000 na hadi sasa amejipatia Pauni 840,000.


EMIL KRAFTH

Lango la  Newcastle linaonekana kuwa kwenye mikono salama mbele ya Nick Pope na hiyo imekuwa ikimnyima nafasi Krafth kuonekana langoni.

Msimu huu amecheza mechi tatu za michuano yote na kwenye EPL amecheza mechi moja tu ambayo pia alicheza kwa dakika moja pekee.

Analipwa mshahara wa Pauni 55,000 kwa wiki na hadi unavyosoma hivi sasa amevuna zaidi ya Pauni 770,000 kwa mechi zake hizo tatu ambazo nyingi aliingia akitokea benchi pia.


CALUM CHAMBERS

Alionekana kwenye mechi mbili za Uefa Conference League. Lakini hajawahi kuitumikia Aston Villa kwenye mechi za EPL na mara zote amekuwa akionekana benchini.

Staa huyu ambaye alijiunga na Villa akitokea Arsenal kwa usajili huru mwaka jana amevuna Pauni 700,000 kutoka Villa. Kila wiki anapata Pauni 50,000.