Mason Greenwood kuipa United mkwanja mzito
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa zamani wa Man United anataka kuondoka Marseille baada ya kuitumikia kwa misimu miwili tangu mwaka 2024.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA wa Marseille Mason Greenwood anatarajiwa kuipa Manchester United kiasi kikubwa cha pesa ikiwa atafanikisha dili lake la kujiunga na Juventus katika dirisha lijalo.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Man United anataka kuondoka Marseille baada ya kuitumikia kwa misimu miwili tangu mwaka 2024.
Uhamisho huo ni habari njema kwa viongozi wa Man United wanaokabiliwa na changamoto za kifedha kwani watapata asilimia kubwa ya ada ya uhamisho wake kutokana na makubaliano waliyoweka na Marseille wakati wanamuuza staa huyo.
Hata hivyo, Greenwood mwenye umri wa miaka 24 ana hofu kuwa sehemu ya fedha itakayochukuliwa na Man United inaweza kuharibu dili hilo kwani viongozi wa Marseille wanaweza kudai ada kubwa zaidi ili kuhakikisha wanabakiwa na pesa nyingi baada ya kuilipa Man United mgao wao.
Chanzo kimoja kilisema: “Mason hana furaha Marseille na ana nia ya kutaka kuhamia Italia kwa sababu pia hataki kurejea Ligi Kuu England.”
Ripoti za ndani zinadai Man United itachukua asilimia 50 ya ada ya uhamisho ambayo Marseille itaipata baada ya kumuuza Greenwood.
Asilimia hizo zinaonekana kuwa nyingi na kuna uwezekano mkubwa Marseille ikahitaji takribani Euro 70 hadi 80 milioni ili kumuuza Greenwood ambapo watabakiwa na walau Euro 35 hadi 40 milioni baada ya kutoa asilimia 50.
Juventus inadaiwa kutaka kujenga upya kikosi chao na kurejea kwenye ushindani baada ya kushindwa kufikia malengo katika misimu ya karibuni na mbali ya Greenwood pia wapo katika mazungumzo na wawakilishi wa nyota wa Real Madrid Antonio Rudiger ambaye inahitajika ajiunge nao mwisho wa msimu ambapo mkataba wake utakuwa unamalizika.