Martinelli apandishiwa mshahara Arsenal

LONDON, ENGLAND. NYOTA wa Arsenal, Gabriel Martinelli amesaini mkataba mnono utakaomweka ndani ya klabu hiyo hadi mwaka 2027 baada ya mazungumzo yaliochukua muda mrefu kufikia makubaliano.

Katika dili jipya, staa huyo wa Kibrazili atakuwa akilipwa mshahara wa Pauni 180,000 kwa wiki kutoka mshahara wake wa awali aliokuwa aliokuwa akilipwa Pauni 70,000 kwa wiki.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta bado ana matumani na Bukayo Saka na William Saliba watafuata nyayo za Martinelli hivi karibuni, kwasababu ndio wachezaji wake muhimu wenye mchango mkubwa kikosini. Mkataba wa Martinelli aliosaini una kipengele cha kuongeza miezi 12 mingine.

Chelsea na Barcelona zilikuwa zikimnyemelea winga huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 21, lakini Martinelli hakuwa na mpango wa kuachana na maisha ya Emirates kwa siku za karibuni.

Sasa Arteta amehamisha nguvu kwa mastaa wake wengine Saka na Saliba ambao mikataba yao itafikia ukingoni mwaka 2024. Mhispania huyo anataka kuhakikisha mastaa wake wanasaini kandarasi jipya haraka iwezekanavyo.

Lakini kwa mujibu wa ripoti Arteta hana haraka kwasababu anaamini Saka na Saliba watasaini mikataba ya kuendelea kukipiga Emirates kwa muda mrefu.

Saliba, Martinelli na Saka wamekiwasha msimu huu Arsenal ikiendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.