Mara paap! Casemiro chama moja na Messi
Muktasari:
- Nyota huyo wa Brazil ataondoka Manchester United mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.
MIAMI, MAREKANI: KIUNGO wa Kibrazili, Casemiro ameripotiwa kuzivutia klabu za Inter Miami pamoja na timu yake ya utotoni nchini Brazil.
Nyota huyo wa Brazil ataondoka Manchester United mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.
Casemiro, anayefikisha miaka 34 wiki ijayo, alionekana akifurahia mapumziko mafupi ya majira ya baridi mjini Miami pamoja na mkewe Anna wiki hii. Inaeleweka kuwa alikuwa Florida kuchunguza mazingira huku akitathmini chaguo zake baada ya Kombe la Dunia 2026.
Miami ni kati ya klabu kadhaa zinazofikiria kumsajili kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid. Klabu hiyo inayomilikiwa na David Beckham imemweka Casemiro juu katika orodha yao ya viungo inaowahitaji baada ya Sergio Busquets kutangaza kustaafu mwaka jana.
Iwapo atahamia klabu hiyo ya Sunshine State, Casemiro ataungana na mpinzani wake wa zamani wa Barcelona, Lionel Messi na kuongeza idadi ya wachezaji waliowahi kucheza na magwiji wawili wa soka, Messi na Cristiano Ronaldo.
Mshindi huyo mara tano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya pia amezivutia klabu za FC Porto na Sao Paulo FC, ambako alijiunga akiwa kijana na kuanza taaluma yake ya soka la kulipwa.
Sao Paulo inatarajiwa kumpa Casemiro mkataba wa miaka miwili pamoja na chaguo la kufanya kazi ndani ya klabu baada ya mkataba wake kumalizika. Saudi Arabia pia ni chaguo jingine na kiwango chake cha sasa kinaonyesha bado ana mengi ya kutoa hasa katika michezo yenye kasi ndogo. Anaweza kuungana tena na Cristiano Ronaldo katika kikosi cha Al-Nassr huku Ligi Kuu ya Saudia ikiendelea kuonyesha nia.
Man United imeamua kutokifanyia kazi kipengele cha kuongeza mwaka mmoja katika mkataba wa Casemiro ulioanza mwaka 2022. Klabu hiyo imedhamiria kuepuka mikataba ya muda mfupi ambayo imeleta matatizo hapo awali. Casemiro ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa fedha nyingi katika kikosi cha Man United, akipokea karibu Pauni 350,000 kwa wiki.
Man United inaendelea kwa kasi kuboresha safu ya kiungo, huku Elliot Anderson, Adam Wharton, Carlos Baleba na Alex Scott wakiwa kwenye rada ya wachezaji inaotaka kuwasajili kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
WACHEZAJI WALIOWAHI KUCHEZA PAMOJA NA MESSI NA RONALDO
Angel Di Maria
Sergio Ramos
Gerard Pique
Gonzalo Higuain
Paulo Dybala
Carlos Tevez
Keylor Navas
Deco
Achraf Hakimi
Alejandro Garnacho
Lisandro Martinez
Vitinha
Nuno Mendes
Danilo Pereira
Gabriel Heinze
Miralem Pjanic
Arthur Melo
Andre Gomes
Nelson Semedo
Francisco Trincao
Renato Sanches
Pablo Sarabia
Henrik Larsson
Martin Caceres
Ezequiel Garay
Fernando Gago
Gonzalo Martinez