MAPYA: Baloteli adai kuna mtu hampendi Anfield
Muktasari:
Balotelli alisugua benchi katika pambano la juzi dhidi ya Burnley ambalo Liverpool walishinda 2-0 katika dimba la Anfield na japo mashabiki walitazamia kocha Brendan Rodgers angemwingiza baadaye, lakini haikuwa hivyo.
SIYO bure kuna mchawi humu ndani, kuna mtu hanipendi. Hivi ndivyo mshambuliaji mtukutu wa Liverpool, Mario Balotelli, alivyoacha fumbo baada ya kuandika ujumbe huo katika mitandao ya kijamii juzi Jumatano usiku.
Balotelli alisugua benchi katika pambano la juzi dhidi ya Burnley ambalo Liverpool walishinda 2-0 katika dimba la Anfield na japo mashabiki walitazamia kocha Brendan Rodgers angemwingiza baadaye, lakini haikuwa hivyo.
Mtaliano huyo ambaye amewahi kuichezea Manchester City, amefunga bao moja tu tangu ahamishwe kwa dau Pauni 16 milioni kutoka AC Milan Agosti mwaka jana baada ya Kombe la Dunia lililofanyika Brazil.
Mara baada ya ushindi dhidi ya Burnley, Balotelli aliandika katika mtandao wake wa Instagram akisema: “Kuna mtu hanipendi”. Hata hiyo hakuweka wazi mtu huyo ni nani.
hata hivyo, baadaye Balotelli aliandika maneno mazuri ya kuwasifia wachezaji wenzake kutokana na ushindi huo huku akitoa madai kwamba yeye ni mchezaji anayecheza kwa ajili ya timu na si mbinafsi.
“Kuna mtu hanipendi lakini tofauti na wanavyosema kuhusu mimi, mimi ni mchezaji wa kitimu na ninajivunia timu yangu, kwa ushindi huu na kwa mashabiki hawa tusonge mbele,” aliongeza kuandika staa huyo wa zamani wa Inter Milan.
Hivi karibuni Balotelli alizua utata baada ya kumpora mpira mikononi mwa nahodha wake, Jordan Henderson na kupiga penalti muhimu katika dakika za majeruhi, penalti hiyo iliipatia Liverpool ushindi dhidi ya Besktas katika Ligi ya Europa.
Hata hivyo, wiki moja baadaye, staa huyo alitolewa katika pambano la marudiano dhidi ya Waturuki hao, lakini Liverpool ilichapwa kwa matuta huku mlinzi, Dejan Lovren, akipoteza penalti muhimu ya mwisho.
Katika pambano la juzi dhidi ya Burnley ambalo Balotelli alisugua benchi, shukrani za pekee zimwendee Henderson aliyefunga bao la kwanza na kupika la pili lililofungwa na mshambuliaji, Daniel Sturridge likiwa ni pambano lake la kwanza tangu atoke benchi la majeruhi.
Ushindi huo umeendelea kuifanya Liverpool izikabe koo timu za Arsenal na Manchester United ambazo zinakamata nafasi za tatu na ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England.