Mane achomoa kuiokoa Senegal isichapwe Afcon 2025
Muktasari:
- Lakini, Senegal ilisawazisha dakika ya 69 kupitia kwa Sadio Mane baada ya Ibrahim Mbaye kumshinda Lionel Mpasi na kupeleka mpira kwa Mane aliyefunga bao la kusawazisha na kufanya ubao usomeke 1-1.
RABAT, MOROCCO: SENEGAL imetokea nyuma kusawazisha bao dhidi ya DR Congo katika mchezo wa Kundi D la Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025, huku timu zote mbili zikikaribia hatua ya 16 bora. Cedric Bakambu aliwafungulia DR Congo bao la kuongoza dakika ya 61 baada ya Edouard Mendy kushindwa kuudaka mpira wa Theo Bongonda.
Lakini, Senegal ilisawazisha dakika ya 69 kupitia kwa Sadio Mane baada ya Ibrahim Mbaye kumshinda Lionel Mpasi na kupeleka mpira kwa Mane aliyefunga bao la kusawazisha na kufanya ubao usomeke 1-1.
Senegal inashika nafasi ya kwanza kwenye kundi hilo ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na DR Congo yenye pointi nne pia, lakini zikitofautina kwenye mabao.
Benin iko nafasi ya tatu na pointi tatu, wakati Botswana iko chini kabisa bila pointi na iko hatarini kutolewa.
Mchezo wa mwisho wa Kundi D utafanyika Jumanne, ambapo Senegal itacheza na Benin huku DR Congo ikicheza na Botswana.
Pointi nne zinatosha kwa timu zote mbili kufuzu hatua ya 16 bora.
Lakini, Benin inatishia nafasi ya mmoja endapo kama itashinda mechi yao ya mwisho kwenye kundi hilo.
Katika mechi ya mapema ya Kundi D, Benin iliandikisha ushindi wake wa kwanza kwenye Afcon 2025 baada kuichapa Botswana 1-0 na hivyo kufanya vita ya kufuzu mtoano kuwa tamu zaidi.