Mancini ajipeleka Man United kiaina
Muktasari:
- Mtaliano huyo mwenye umri wa miaka 60 kwa sasa hana kazi tangu alipoachana na Saudi Arabia mwaka jana, lakini amewaambia marafiki zake anaamini anaweza kwenda kupiga kazi Man United endapo kama fursa hiyo itapatikana.
MILAN, ITALIA: KOCHA Roberto Mancini amewaambia marafiki zake anaweza kuwa chaguo la kushtua wengi la kutua Manchester United wakati itakapomfuta kazi Ruben Amorim.
Mtaliano huyo mwenye umri wa miaka 60 kwa sasa hana kazi tangu alipoachana na Saudi Arabia mwaka jana, lakini amewaambia marafiki zake anaamini anaweza kwenda kupiga kazi Man United endapo kama fursa hiyo itapatikana.
Kama ilivyo kwa bilionea mmiliki mwenza wa Man United, Sir Jim Ratcliffe, Mancini maskani yake ipo kusini mwa Ufaransa na imeleezwa amekuwa akikutana na bilionea huyo nwa kampuni ya Ineos kwenye shughuli mbalimbali za kijamii huko kwenye makazi yao.
CV ya Mancini haina mashaka, alinyakua mataji alipokuwa Etihad kuinoa Manchester City na aliipa Italia taji la Euro 2020, tena mbele ya England.
Mashabiki wa Man City wanamtazama Mancini kama shujaa wao baada ya kuisaidia timu hiyo kumaliza ukame wa miaka 34 wa kubeba taji, alipowapa ubingwa 2011 na aliwapa taji nyingine mwaka uliofuatia.
Mancini aliondolewa Man City mwaka 2013 baada ya kuinoa timu hiyo katika mechi 191. Katika kikosi cha Etihad, alishinda mechi 113 na kuchapwa 40.
Mtaliano huyo alikwenda kuzinoa pia Galatasaray, Inter Milan, Zenit Saint Petersburg, Italia na Saudi Arabia. Mancini si kocha pekee anayehusishwa na kibarua cha kuinoa Man United.