Man Utd yapewa masharti kwa Mbeumo

Muktasari:
- Man United inamtaka Mbeumo na huenda akaenda kuungana na Ollie Watkins baada ya miamba hiyo ya Old Trafford kumweka kwenye orodha ya wachezaji inaowataka dirisha hili straika huyo wa Aston Villa.
LONDON, ENGLAND: BRENTFORD imeiambia Manchester United inapaswa kulipa Pauni 65 milioni kama kweli inamtaka Bryan Mbeumo kinyume cha hapo, fowadi huyo atabaki, haendi kokote.
Man United inamtaka Mbeumo na huenda akaenda kuungana na Ollie Watkins baada ya miamba hiyo ya Old Trafford kumweka kwenye orodha ya wachezaji inaowataka dirisha hili straika huyo wa Aston Villa.
Brentford imegomea ofa mbili za Man United, ikiwamo ya Pauni 60 milioni kwa ajili ya Mcamerooni Mbeumo.
Mazungumzo yanaendelea baina ya klabu hizo mbili, lakini mkurugenzi wa soka wa Brentford, Phil Giles alifichua kwamba Mbeumo anaweza kubaki hadi msimu ujao. Mbeumo alifunga mabao 20 msimu uliopita. Ofa ya mwisho ya Man United iliyopelekwa Brentford ni Pauni 55 milioni zitakazolipwa awali na Pauni 5 milioni kama nyongeza.
Giles, ambaye alithibitisha kuhusu nahodha Christian Norgaard kwenda Arsenal kwa Pauni 9.3 milioni, alisema: “Kama wachezaji wataondoka, basi kwa matakwa yetu. Mabao 20 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita kwa Mbeumo, tulitarajia kupata maombi mengi na hakika tumepokea maombi mengi. Kama ataondoka, basi hilo litakuwa limetupatia pesa za kutosha sisi, tumekuwa wazi kwenye hilo.
“Lakini, kama ataendelea kubaki hapa hadi msimu ujao, sitashangaa. Tutakuwa wenye furaha. Na hilo si kwamba halipo kwenye meza yetu, acha tusubiri tuone itakavyokuwa.”
Mbeumo, 25, anataka kuhamia Old Trafford. Na straika wa zamani wa Brentford, Watkins, 29, naye amewekwa kwenye mipango ya Man United endapo itamuuza mshambuliaji Rasmus Hojlund.