Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man United yaweka mzigo kwa Bruno Fernandes

Muktasari:

  • Hata hivyo, supastaa huyo mwenye umri wa miaka 31 anadaiwa kuweka wazi kuwa ataamua mustakabali wake ndani ya viunga hivyo mwisho wa msimu huu kwani anataka kuona ikiwa watafuzu kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao au la.

MANCHESTER United ipo tayari kumpa kiungo wake wa kimataifa wa Ureno, Bruno Fernandes, ofa mpya ya mkataba itakayomuingizia mshahara wa hadi Pauni 400,000 kwa wiki.

Hata hivyo, supastaa huyo mwenye umri wa miaka 31 anadaiwa kuweka wazi kuwa ataamua mustakabali wake ndani ya viunga hivyo mwisho wa msimu huu kwani anataka kuona ikiwa watafuzu kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao au la.

Ikiwa Mashetani Wekundu watashindwa kufikia lengo hilo kuna uwezekano mkubwa Fernandes akaangalia chaguo jingine licha ya dau nono lililopo mezani.

Nahodha huyo wa sasa wa Man United amekuwa akihusishwa na timu za Saudi Arabia ambazo mwaka jana zilikuwa tayari kumpa mshahara wa hadi Pauni 800,000 kwa wiki, lakini alikataa na kubaki Man United kwa sababu aliamini kwamba bado anahitaji kuendelea kucheza soka la ushindani.

Mkataba wa Fernandes unatarajiwa kumalizika 2027 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 27 za michuano yote akifunga mabao saba na kutoa asisti 14.


Kobbie Mainoo

HATMA ya kiungo wa kimataifa wa England, Kobbie Mainoo, mwenye umri wa miaka 20, ndani ya Manchester United bado haijafahamika, huku mazungumzo ya mkataba mpya yakiendelea kufanyika. Taarifa zinaeleza kuwa pande husika hazijafikia mwafaka juu ya masuala ya kifedha na muda wa mkataba, ingawa taarifa za ndani zinadai benchi la ufundi la Mashetani Wekundu linahitaji kuona akiendelea kusalia katika kikosi. Mkataba wake unaisha 2027.


Micky van de Ven

BARCELONA inatarajiwa kutuma ofa kwa Beki wa Tottenham Hotspur, Micky van de Ven, 24, mwisho wa msimu. Taarifa zinaeleza kuwa Barca inamchukulia beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi kama chaguo sahihi la kuimarisha safu ya ulinzi kutokana na kiwango alichoonyesha msimu huu. Hata hivyo, dili hilo halitakuwa rahisi kwani Spurs inathamini mchango wake kikosini na huenda ikahitaji dau kubwa kabla ya kumruhusu kuondoka.


Fabio Carvalho

BRENTFORD imeanza mipango ya kufanya marekebisho makubwa katika kikosi kuelekea msimu ujao baada ya kuamua kuuza wachezaji watano akiwemo kiungo wa kimataifa wa Ureno, Fabio Carvalho, 23. Taarifa zinaeleza kuwa uongozi unaangalia uwezekano wa kuuza au kuachia baadhi ya nyota ili kupunguza mzigo wa mishahara na kuacha nafasi ya kusajili wachezaji wapya watakaoendana na mipango.


Pio Esposito

ARSENAL imeambiwa kuwa mshambuliaji wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, Pio Esposito, mwenye umri wa miaka 20, hauzwi kwa bei yoyote. Mabosi walishatuma hadi maskauti kwa ajili ya kumtazama staa huyo akicheza na walionekana kuvutiwa naye, hivyo wakapanga kufanya usajili wake katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini sasa mpango huo unaonekana kushindikana.


Mason Mount

MANCHESTER UNITED imesisitiza haina mpango wa kumuuza kiungo wa kimataifa wa England, Mason Mount, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya Aston Villa na Fulham kuonyesha nia ya kumsajili. Uongozi wa Mashetani Wekundu unaamini Mount ana nafasi katika mipango ya muda mrefu ya klabu licha ya kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara yaliyomzuia kuonyesha uwezo wake tangu ajiunge na timu hiyo.


Dusan Vlahovic

JUVENTUS inaonekana kupiga hatua kubwa katika mazungumzo ya kumwongeza mkataba mshambuliaji wake wa kimataifa wa Serbia, Dusan Vlahovic, mwenye umri wa miaka 26, ambao kwa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Taarifa zinaeleza uongozi wa Juventus unatambua umuhimu wa straika huyo katika kikosi na hautaki aondoke bure. Tangu msimu uanze amecheza mechi 17.


Konrad Laimer

BAYERN MUNICH imesitisha kwa muda mazungumzo ya mkataba mpya na kiungo wa kimataifa wa Austria, Konrad Laimer, 28, baada ya staa huyo kuhitaji kiasi kikubwa cha pesa. Inaelezwa kuna pengo kubwa kati ya kiasi ambacho anahitaji na kile ambacho Bayern Munich iko tayari kutoa, jambo lililosimamisha mazungumzo. Hata hivyo, kuna uwezekano wa mazungumzo kurejea. Mkataba unamalizika 2027.