Man United yamtibulia shabiki kunyoa nywele
Muktasari:
- Jamaa huyo mwenye nywele nyingi alitarajia Man United ipate ushindi dhidi ya West Ham United, Jumanne usiku, lakini ilishindikana baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu England iliyofanyika huko London kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
MANCHESTER, ENGLAND: HABIKI mwenye nywele nyingi wa Manchester United, Frank Illett amebaki hana la kusema huku akisubiri karibu siku 500 kukata nywele zake baada ya mkeka alioweka kushindwa kutiki.
Jamaa huyo mwenye nywele nyingi alitarajia Man United ipate ushindi dhidi ya West Ham United, Jumanne usiku, lakini ilishindikana baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu England iliyofanyika huko London kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Alikuwa na matumaini ya kunyoa nywele zake za mawimbi zinazofanana na wigi endapo kama Man United ingeibuka na ushindi wa tano mfululizo, lakini haikufanikiwa. Illett alikuwa ameahidi kukata nywele zake ndefu na zisizo za kawaida pale tu Man United watakaposhinda mechi tano mfululizo.
Kocha wa muda, Michael Carrick aliiongoza Man United kushinda mechi nne mfululizo kabla ya safari ya kwenda Uwanja wa London usiku huo.
Illett alikuwa tayari ameshika mashine ya kunyoa akifanya matangazo ya moja kwa moja (live watch-along) mbele ya watazamaji zaidi ya 150,000, huku idadi ya watazamaji ikifikia 265,000 mwishoni mwa mechi.
Lakini, ndoto yake ya kunyoa nywele ilififia pale Man United iliponusurika kichapo kwa kulazimisha sare ya 1-1 Mashariki mwa London. Bao la Tomas Soucek katika dakika ya 50 lilimwacha Illett akiwa mdomo wazi akitambua atalazimika kuendelea kuishi na nywele zake hizo nyingi.
Shabiki huyo wa Man United alidhani laana ilikuwa karibu kuvunjika wakati Casemiro aliposawazisha kwa upande wake. Hata hivyo, bao la Mbrazili huyo lilikataliwa na VAR na kuvunja matumaini ya Illett. Kulikuwa na mwanga wa matumaini mwishoni wakati Benjamin Sesko alipofunga bao zuri kwa Man United ikiwa imesalia dakika moja ya muda wa majeruhi. Lakini, ilikuwa imechelewa mno, huku West Ham wakishikilia sare hiyo nyumbani. Illett alionekana kushika kichwa chake kwa mikono baada ya mwisho wa kusisimua wa mechi.
Alitikisa afro yake kubwa kwa masikitiko huku akitambua hali halisi kabla ya kusema kwa msisitizo: “Nimefika mbali sana kuja kukata tamaa sasa.” Sasa Man United italazimika kuanza tena safari ya kushinda mechi tano mfululizo kabla mashine ya kunyoa haijatoka. Watapata nafasi ya kuanza upya Jumatatu ijayo watakapokwenda kucheza dhidi ya Everton. Lakini bado haijulikani nywele za Illett zitakuwa ndefu kiasi gani, kwani tayari amekaa karibu miaka miwili bila kushikwa na kinyozi. Mara ya mwisho alikata nywele Oktoba 2024, akiapa kuzikuza hadi Man United washinde mechi tano mfululizo. Nywele zake kwa sasa zina urefu wa sentimita 25.