Man United yaanza mazungumzo ya Varane

LONDON, ENGLAND. KLABU ya Manchester United imeripotiwa kuingia kwenye mazungumzo na  Real Madrid ya kumsajili beki wa timu hiyo na taifa la Ufaransa, Raphael Varane.

Ole Gunnar Solskjaer  ameonyesha kuwa na nia ya kutaka kusajili beki mwengine wa kati ambaye atakuwa akicheza na  Harry Maguire msimu ujao.

Licha ya kwamba Victor Lindelof alikuwa akicheza na  Maguire kwenye michezo mingi ya Manchester United msimu uliopita, kocha huyo ameamua kufanya maboresho zaidi.

Varane ndiye chaguo la kwanza kwa kocha huyo, mkataba wa Varane na Real Madrid umebakiwa mwaka mmoja hivyo miamba hiyo ya Hispania itawalazimu kumuuza beki huyo ili asije kuondoka bure mara baada ya mkataba wake kumalizika, 2022.

Real Madrid wanakumbukumbu za kumpoteza bure aliyekuwa nahodha wao, Sergio Ramos  ambaye ametimkia zake Ufaransa kwa kujiunga na Paris SG.

Kwa mujibu wa  ripoti ni kwamba Manchester United imeanza mazungumzo rasmi na Real Madrid kwa ajili ya kufanya makubaliano ya uhamisho huo.

Hivi karibuni iliripotiwa kwamba Varane ameonyesha utayari wa kujiunga na mashetani wekundu hao wa Old Trafford, anaonekana kuwa mwenye shauku ya kutaka kukabiliana na changamoto mpya kwenye Ligi ya England maarufu kama EPL.