Man United, Liverpool zinapigana vikumbo kwa Branthwaite
Muktasari:
- Branthwaite, ambaye msimu uliopita alicheza mechi 35 za Ligi Kuu England na kufunga mabao matatu, anahitajika na vigogo hao kwa ajili ya kuboresha safu zao za ulinzi.
LIVERPOOL na Manchester United zinaiwania saini ya beki kisiki raia wa England, Jarrad Branthwaite, 23, kutoka Everton dirisha lijalo la majira ya baridi.
Branthwaite, ambaye msimu uliopita alicheza mechi 35 za Ligi Kuu England na kufunga mabao matatu, anahitajika na vigogo hao kwa ajili ya kuboresha safu zao za ulinzi.
Ripoti zinaeleza Everton ipo tayari kumuuza staa huyu kwa Pauni 65 milioni, ingawa kuhitajika kwake na timu nyingi kunaweza kusababisha bei yake ikapanda.
Liverpool inamwangalia staa huyu baada ya kuona kuna ugumu katika dili la Marc Guehi ambaye hivi karibuni ripoti zilidai amewaambia wawakilishi wake kwamba angependa zaidi kujiunga na Real Madrid badala ya Liverpool.
Madrid imeingia katika mchakato wa kumsajili Guehi baada ya kuona mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu. Liverpool ilikuwa karibu kumsajili lakini ilifeli katika dakika za mwisho za dirisha lililopita la usajili.
Man United ambayo imeanza vibaya msimu huu, imekuwa ikimwinda fundi huyu kwa muda mrefu na changamoto iliyosababisha isiwe imemsajili hadi sasa ni ada yake ya uhamisho.
Conor Gallagher
MANCHESTER United inajipanga kumsajili kiungo wa kati wa Atletico Madrid, Conor Gallagher, mwenye miaka 25. Gallagher anadaiwa kutamani sana kurejea England na Atletico ipo tayari kumuuza kwa ada ya uhamisho wa takribani Pauni 40 milioni. Man United inamwona fundi huyu kama mbadala wa Casemiro ambaye kuna uwezekano mkubwa akaondoka mwisho wa msimu huu na inapambana kuimarisha kikosi chao ambacho kinasuasua Ligi Kuu England.
Mason Greenwood
ATLETICO Madrid inataka kumsajili mshambuliaji wa Marseille, Mason Greenwood, 23, dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini inaonekana kuwa ngumu kuipata huduma yake. Marseille bado inahitaji huduma ya fundi huyu na kocha Roberto de Zerbi anamwona kama sehemu muhimu ya mipango yake. Mkataba wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, na msimu huu amecheza mechi saba za michuano yote na kufunga mabao mawili.
Joe Gomez
AC Milan imevutiwa sana na beki wa kati wa Liverpool, Joe Gomez, 28, na inataka kumsajili dirisha lijalo la majira ya baridi. Milan imeonyesha nia kwa sababu Gomez sio mchezaji tegemeo wa kikosi cha Liverpool kwa sasa na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi tatu tu, mbili za Ligi Kuu England ambazo zote aliingia akitokea benchi na moja ya Carabao Cup aliyocheza kwa dakika zote. Mkataba wake na Liverpool unamalizika 2027.
Nico Paz
CHELSEA ina matumaini makubwa ya kuipiku Real Madrid katika mbio za kuiwania saini ya kiungo Como, Nico Paz, 21, dirisha lijalo. Paz ambaye alitua Como mwaka jana akitokea timu ya vijana ya Madrid amekuwa katika kiwango bora sana msimu huu na katika mechi sita alizocheza amefunga mabao matatu na asisti tatu. Chelsea inahitaji kuongeza nguvu eneo lao la kiungo ambalo mara kadhaa kumeonekana kuna mapungufu.
Karim Benzema
BENFICA inayofundishwa na Kocha Jose Mourinho, ipo karibu kufikia makubaliano na mshambuliaji wa Al-Ittihad ya Saudi Arabia, Karim Benzema, 37. Inaelezwa Mourinho ndio anasimamia mchongo wote na Benzema anataka kutua Benfica kutokana na heshima kubwa ambayo anayo kwa kocha huyo. Mara kadhaa Benzema amekuwa akiweka wazi Mourinho ndiye aliyebadilisha maisha yake baada ya kutua Madrid.
Dayot Upamecano
LIVERPOOL inaangalia uwezekano wa kumsajili beki wa kati wa Bayern Munich, Dayot Upamecano, 26, kwa usajili huru dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Upamecano, ambaye mkataba wake unamalizika Juni 2026, ameripotiwa kugoma kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Bayern kwa sababu anahitaji changamoto mpya sehemu nyingine.
Manuel Locatelli
CHELSEA inapanga kutuma ofa Juventus kumnunua kiungo wao, Manuel Locatelli, 27, mwisho wa msimu. Hata hivyo, inakumbana na upinzani mkali kutoka Newcastle United, Aston Villa, West Ham United na Bayer Leverkusen zinazohitaji saini yake. Locatelli, aliyewahi kushinda Kombe la Euro 2020 akiwa na Italia, ni miongoni mwa mihimili muhimu ya Juventus.