Upamecano atua anga za Real Madrid, mchongo upo hivi
Muktasari:
- Real Madrid inataka kujenga safu mpya ya ulinzi na kwa sasa inaundwa na mastaa ambao umri unaenda kuwatupa mkono pia wamekuwa wakisumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara.
REAL Madrid inapanga kumsajili beki kisiki wa kimataifa wa Ufaransa, Dayot Upamecano, 26, ambaye yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake na Bayern Munich.
Real Madrid inataka kujenga safu mpya ya ulinzi na kwa sasa inaundwa na mastaa ambao umri unaenda kuwatupa mkono pia wamekuwa wakisumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara.
Bayern inapambana sana kutaka kumsainisha mkataba mpya lakini anaonekana hana mpango wa kuendelea kusalia katika kikosi hicho na badala yake anataka kuondoka kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.
Ikiwa ataendelea kugoma kusaini mkataba mpya, Bayern imepanga kumuuza Januari lakini kwa kiasi kisichopungua Euro 30 milioni.
PSG pia inataka huduma yake lakini Madrid ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kumsajili kwani imeshaanza hadi mazungumzo na wakala wake.
Beki huyu aliyejiunga na Bayern mwaka 2021 akitokea RB Leipzig, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi nane za michuano yote na kutoa asisti moja.
Federico Chiesa
LIVERPOOL haitaki kumruhusu mshambuliaji wao wa kimataifa wa Italia, Federico Chiesa, kuondoka dirisha hili licha ya kutomjumuisha katika kikosi kitakachocheza Ligi ya Mabingwa msimu huu. Staa huyu anahitajika na Besiktas ya Uturuki ambayo ipo tayari kumsajili dirisha hili. Liverpool haitaki kumuuza staa huyu mwenye umri wa miaka 27, ingawa inadiawa anatamani kuondoka na kocha Arne Slot amezuia kwa sababu anataka kumtumia katika mashindano mengine.
Stefan Ortega
KIPA wa Manchester City na timu ya taifa ya Ujerumani, Stefan Ortega, 32, sasa huenda akaendelea kubaki Manchester City hadi Januari baada ya Trabzonspor kuamua kumsajili kipa wa Manchester United na timu ya taifa ya Cameroon, Andre Onana, 29, badala yake. Ortega alikuwa chaguo la pili nyuma ya Ederson, lakini Pep Guardiola anamwona kama kipa muhimu wa michuano ya Kombe la FA na Carabao na anataka abaki hususani baada ya Ederson kuondoka.
Angelo Stiller
ARSENAL iko mstari wa mbele katika harakati za kutaka kumsajili kiungo wa Stuttgart, Angelo Stiller, 24, dirisha lijalo la majira ya baridi. Staa huyu alikuwa akiwindwa na Manchester United ambayo jaribio lao la dakika za mwisho la kutaka kumsajili katika dirisha lililopita la usajili liligonga mwamba. Licha ya Arsenal kuonekana kama ina nafasi kubwa, Bayern Munich (klabu aliyowahi kuchezea katika akademi) na Real Madrid pia zinamfuatilia kwa karibu ili kumnasa dirisha lijalo.
Senny Mayulu
TOTTENHAM ilifanya jaribio la dakika za mwisho kumsajili kiungo chipukizi wa PSG, Senny Mayulu, 19, kabla dirisha kufungwa lakini ilishindikana. Inaelezwa Spurs bado haijakata tamaa na inataka kujaribu tena dirisha lijalo ingawa itakumbana na upinzani kutoka kwa Chelsea na Manchester City ambazo zinahitaji saini yake pia. PSG ilikuwa tayari kumwachia fundi huyu lakini kwa mkopo kwa sababu inamwona kama sehemu ya mipango yao ya muda mrefu hivyo haitaki kumuuza moja kwa moja.
Jorgen Strand Larsen
WOLVES ina uhakika wa asilimia mia wa kumsainisha mkataba mpya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Norway, Jirgen Strand Larsen, 25, katika wiki kadhaa zijazo. Katika mkataba huo mpya itaweka kipengele cha kumwachia kwa dau maalum (release clause). Katika dirisha lililopita Wolves ilikataa ofa mbili za zaidi ya Pauni 50 milioni kutoka Newcastle kwa ajili ya staa huyu. Strand Larsen alisajiliwa na Wolves kutoka Celta Vigo mwaka 2024.
Daniel Vivian
Newcastle, Man United na Aston Villa zinainyemelea saini ya beki wa kati wa Athletic Bilbao, Daniel Vivian, 26, ambaye inataka kuwasalisha ofa kwa ajili ya kumsajili dirisha lijalo la majira ya baridi. Inaelezwa katika mkataba wa fundi huyu kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa takribani Pauni 35 milioni. Vivian ni sehemu muhimu ya safu ya ulinzi ya Bilbao na hadi sasa ameitwa mara mbili katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Hispania.
Mike Maignan
CHELSEA bado ina nia ya kumsajili kipa wa AC Milan Mike Maignan, 30, licha ya kushindwa kufikia makubaliano dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Inaelezwa matajiri hao wa Jiji la London, wanataka kusubiri hadi mwisho wa msimu huu ili kumsajili bure kwani mkataba wake utakuwa unamalizika. Maignan ambaye amekuwa akiichezea timu ya taifa ya Ufaransa, alishinda Serie A na Milan mwaka 2022.