Man United haivunji benki kwa straika mpya
Muktasari:
- Mashabiki wa Man United wanaamini kwamba kitendo cha Alexander Isak kuwaambia Newcastle kwamba anataka kuondoka St James’ Park hilo linaweza kuwahamasisha mabosi wa Old Trafford wakatunisha msuli kumchukua.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeamua kufuta mpango wa kuvunja benki kwa ajili ya kunasa huduma ya mshambuliaji Namba 9 kwenye dirisha hili.
Mashabiki wa Man United wanaamini kwamba kitendo cha Alexander Isak kuwaambia Newcastle kwamba anataka kuondoka St James’ Park hilo linaweza kuwahamasisha mabosi wa Old Trafford wakatunisha msuli kumchukua.
Man United imetumia pesa nyingi kuwanasa Matheus Cunha na Bryan Mbeumo, ikitumia Pauni 130 milioni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, hivyo timu hiyo haipo kwenye nafasi ya kufanya matumizi mengine makubwa labda kama kutakuwa na wachezaji wengi wa kuondoka.
Man United iliwakosa mastraika Liam Delap na Viktor Gyokeres, waliochagua kwenda Chelsea na Arsenal mtawalia. Na imekuwa ikiwawinda Benjamin Sesko na Ollie Watkins na inaelezwa kumfukuzia Msenegali, Nicolas Jackson.
Lakini, sasa Man United imedai haina mpango wa kutumia nguvu nyingi kwenye kufukuzia straika mpya, ikiamini Rasmus Hojlund anaweza kufanya vizuri akicheza na Mbeumo na Cunha na kitakachofanyika kwa sasa ni kumtazama kwenye mechi za kirafiki dhidi ya West Ham, Bournemouth na Everton.
Hojlund, ambaye ameshindwa kuonyesha thamani ya pesa aliyosajiliwa Pauni 72 milioni, akifunga mabao 14 katika mechi 62 alizocheza kwenye ligi tangu alipojiunga na Man United akitokea Atalanta na kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi amekuwa akihusishwa na timu za Juventus, Napoli, Milan, Inter na AS Roma, zikimsaka arudi kukipiga huko Italia.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim, anataka kumpa nafasi ya mwisho straika huyo kuonyesha kama kweli anastahili kubaki Old Trafford.
Anachoamini kocha huyo Mreno kwamba ujio wa Cunha na Mbeumo utaipa Man United nguvu mpya kwenye ushambuliaji na hilo linaweza kumfanya Hojlund awe tishio mbele ya goli kuanzia sasa. Kuna ripoti zinadai, Watkins anaweza kutua Man United kwenye dili la kubadilishana na mchezaji Alejandro Garnacho, ambaye ataenda upande wa pili, Aston Villa.