Man City, Madrid vita kwa Wirtz
Muktasari:
- Man City na Real Madrid ambao wamekuwa wapinzani wakubwa kwa miaka ya karibuni na usiku wa Jumatano, zitarudiana kwenye mechi ya kuwania kutinga hatua ya 16 bora kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, vita yao itahamia kwenye usajili mwishoni wa msimu kwa kumtaka Mjerumani huyo.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City inajiandaa kuchuana jino kwa jino na Real Madrid kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kuwania saini ya kiungo wa Pauni 85 milioni, Florian Wirtz.
Man City na Real Madrid ambao wamekuwa wapinzani wakubwa kwa miaka ya karibuni na usiku wa Jumatano, zitarudiana kwenye mechi ya kuwania kutinga hatua ya 16 bora kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, vita yao itahamia kwenye usajili mwishoni wa msimu kwa kumtaka Mjerumani huyo.
Staa huyo wa Bayer Leverkusen, Wirtz, 21, inaaminika yupo tayari kwenda kukipiga Hispania kama itafika wakati ambao atataka kuhama kutoka kwenye nchi yake ya Ujerumani.
Lakini, Pep Guardiola na mabosi wake wa huko Etihad wanamtazama Wirtz kama mchezaji mwafaka wa kwenda kurithi buti za Kevin De Bruyne.
Man City imeanza kujijenga upya na kwenye dirisha la Januari ilitumia Pauni 175 milioni kunasa mastaa wapya, akiwamo kiungo Nico Gonzalez na mfungaji wa hat-trick, Jumamosi iliyopita, Omar Marmoush.
Lakini, inafahamu wazi De Bruyne, atakayetimiza umri wa miaka 34 mwishoni mwa msimu na mkataba wake utafika tamati katika kipindi hicho. Kocha Guardiola alikiri majeraha ya muda mrefu yamemfanya kiungo huyo wa Kibelgiji asiwe kwenye kiwango chake kama zamani.
Phil Foden anaweza kuziba pengo lake kwa sasa, lakini miamba hiyo ya Etihad, inamtaka Wirtz, ambaye amekuwa muhimu huko Leverkusen msimu huu kwenye kikosi cha Xabi Alonso aende kuvaa uzi wa Etihad.