Man City, Arsenal kama Yanga, Simba

LONDON, ENGLAND. Robo fainali ndipo palikuwa mwisho wa safari kwa miamba ya soka ya Tanzania, Yanga na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Tanzania iliingiza timu mbili kwenye hatua hiyo sawa na England kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester United na Arsenal.

Yanga ilitolewa hatua hiyo na Mamelodi Sundowns kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza timu hizo kutoka suluhu, huku Simba ikiondoshwa na Al Ahly kwa jumla ya mabao 3-0 na mchezo wa mkondo wa kwanza ilifungwa bao 1-0 kabla ya kwenda kufungwa mabao 2-0 ugenini na kuaga michuano.

Sawa na kilichotokea kwa timu za England na Man City iliondoshwa kwenye hatua hiyo kwa kuchapwa mikwaju 4-3 na Real Madrid, baada ya kutoshana nguvu ya bao 1-1 katika dakika 90, huku Arsenal ikiondoshwa kwa bao 1-0 na Bayern Munich.

Hiyo ilikuwa ni michezo ya mkondo wa pili baada ya ule wa kwanza wiki moja iliyopita Arsenal ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Emirates ililazimishwa sare ya mabao 2-2, huku Man City ambao ndio mabingwa watetezi wa kombe hilo, ikilazimisha sare ya mabao 3-3 ugenini kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Katika mchezo huo uliopigwa Etihad, mabao ya timu hizo yalifungwa na Rodrygo dakika ya 12 na la Man City lilifungwa na Kevin de Bruyne dakika ya 76.

Madrid na Bayern sasa zitakutana kwenye nusu fainali ya michuano hiyo huku michezo mingine iliyopigwa juzi na kushuhudiwa Borussia Dortmund itakayokutana na PSG, iliitoa Atletico Madrid kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya Jumanne usiku vijana wa Diego Simeone kushinda nyumbani mabao 2-1, kabla ya kufungwa ugenini mabao 4-2.

PSG ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Barcelona jumla ya mabao 6-4 na mchezo wa kwanza Barca ilishinda mabao 3-2 ugenini kabla ya kufungwa nyumbani Jumanne usiku kwa mabao 4-1.

Michezo hiyo ya nusu fainali itapigwa Mei 7 naMadrid itakuwa nyumbani mchezo wa kwanza sawa na PSG na zitapigwa muda mmoja, saa 4:00 usiku.