Majeruhi wamtia presha Arteta
Muktasari:
- Lakini kupunguzwa kwa pengo la pointi kileleni sio presha pekee anayokumbana nayo
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imepoteza mechi yake ya kwanza tangu Septemba baada ya kulala 2-1 dhidi ya Aston Villa Jumamosi na kuleta presha katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
Lakini kupunguzwa kwa pengo la pointi kileleni sio presha pekee anayokumbana nayo kocha Mikel Arteta.
Kijasho kinamtoka kocha huyo Mhispaniola kutokana na kusambaratika kwa safu yake ya ulinzi kwa sababu ya majeraha
Beki wa Arsenal, Cristhian Mosquera, anaripotiwa kuwa huenda atakuwa nje ya uwanja kwa angalau wiki sita baada ya kupata jeraha katika ushindi wao dhidi ya Brentford siku ya Jumatano.
The Gunners walianza msimu kwa kiwango cha juu, wakiwa kileleni mwa Ligi ya Kuu England na Ligi ya Mabingwa (Hatua ya Makundi).
Fomu yao imekuwa ya kuvutia zaidi kutokana na idadi ya majeraha na wachezaji waliokosekana msimu huu.
Wachezaji kama Martin Odegaard, Noni Madueke, Bukayo Saka na Viktor Gyokeres wote walipata majeraha na kukosa mechi kadhaa kabla ya kurejea, ilhali Gabriel Magalhaes na William Saliba ambao ndio pacha yao la ulinzi, kwa sasa wote ni majeruhi pamoja na Kai Havertz. Leandro Trossard, alirejea kutoka kuwa majeruhi jana na kufunga bao la kusawazisha baada ya Matty Cash kuitanguliza Aston Villa uwanjani Villa Park kabla ya Emiliano Buendia kuweka chuma cha ushindi katika dakika ya mwisho ya mechi.
Kwa mujibu wa BBC Sport, Mosquera sasa atajiunga na orodha ya majeruhi wa kipindi kirefu kutokana na jeraha la kifundo cha mguu alilopata dhidi ya Brentford. Majeraha hayo ya Mosquera yanamfanya Arteta kubaki na beki mmoja tu wa kati wa asili, Piero Hincapie, hiyo inatokana na kutokuwapo kwa uhakika wa kuhusu ufiti wa William Saliba.
Saliba alikosa mechi tatu zilizopita dhidi ya Chelsea, Brentford na Aston Villa, baada ya kuumia mazoezini. Na beki mwingine wa kati, Mbrazili Gabriel Magalhaes amekuwa nje ya uwanja tangu mwezi uliopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya paja.